Katika miongo ya hivi karibuni, Bara la Afrika limeendelea kushuhudia wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika baadhi ya nchi zake, hali inayozua maswali kuhusu uimara wa demokrasia, utawala bora na uhuru wa kisiasa.

Ingawa mapinduzi haya mara nyingi huwasilishwa kama hatua za kurejesha utulivu au kupambana na uongozi mbovu, mwanazuoni wa siasa za Afrika Profesa Nic Cheeseman wa Chuo Kikuu cha Birmingham katika moja ya maandiko yake anasema mara nyingi chanzo chake ni udhaifu wa taasisi za kidemokrasia na migogoro ya uhalali wa kisiasa.

Moja ya dhana muhimu katika kuelewa hali hiyo ni ukoloni mamboleo. Anasema hiyo ni hali ambayo nchi zilizoendelea zinaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa, uchumi na rasilimali za nchi za Afrika hata baada ya kupata uhuru wa kisiasa.

Ushawishi huu mara nyingi hujidhihirisha kupitia mikataba isiyo na usawa, utegemezi wa kiuchumi na wakati mwingine kuingilia moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja katika masuala ya ndani ya nchi.

Wakati mwanazuoni huyo akiyasema hayo, mchumi kutoka Oxford, Profesa Paul Collier aliwahi kusema kuwa utegemezi wa kiuchumi wa Afrika unaendelea kuathiri uwezo wa nchi nyingi kujenga mifumo imara ya kisiasa.

Historia inaonesha baada ya mataifa mengi ya Afrika kupata uhuru katikati ya karne ya 20, matumaini ya kujenga mifumo imara ya kidemokrasia yalikuwa makubwa.

Hata hivyo, anasema katika baadhi ya nchi, matumaini hayo yalivurugwa na mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea mara kwa mara. Hata hivyo, inaelezwa kuwa udhaifu wa taasisi za kiraia na ukosefu wa demokrasia thabiti vilichangia sana kurudi kwa utawala wa kijeshi katika baadhi ya mataifa.

Baadhi ya watafiti wanaeleza kuwa mapinduzi haya yalichochewa na mazingira ya kisiasa yaliyokuwa dhaifu, lakini pia hayakuwaza kutenganishwa na ushawishi wa nje uliokuwa na maslahi ya kiuchumi na kimkakati.

Katika muktadha wa ukoloni mamboleo, mapinduzi ya kijeshi yanaweza kuonekana kama matokeo ya mfumo mpana unaozalisha utegemezi na udhaifu wa taasisi za ndani.

Nchi ambazo hazina uhuru kamili wa kiuchumi, mara nyingi hukumbwa na migogoro ya kisiasa inayoweza kutoa mwanya kwa jeshi kuingilia kati.

Aidha, katika baadhi ya matukio kumekuwapo madai ya kuungwa mkono kwa siri kwa mapinduzi hayo ili kulinda maslahi ya kigeni.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya siasa kama Profesa Samuel Decalo (mchambuzi wa historia ya mapinduzi Afrika) anasema si sahihi kuelezea mapinduzi ya kijeshi kwa kuzingatia ukoloni mamboleo pekee, kwa kuwa sababu za ndani zina mchango mkubwa.

Miongoni mwa sababu hizo ni rushwa, udikteta na tamaa ya madaraka. Katika nchi ambako rasilimali za umma zinatumika vibaya, haki na usawa havipo na viongozi wanashikilia madaraka kwa muda mrefu bila uwajibikaji na hujengwa mazingira yanayochochea kutoridhika kwa wananchi.

Utawala wa kiimla, kwa mfano, mara nyingi hujenga mazingira ya udhaifu wake mwenyewe. Serikali inapozuia uhuru wa kujieleza, kukandamiza upinzani na kudhoofisha taasisi za kikatiba, huondoa njia za amani za mabadiliko ya kisiasa.

Hali hii inaweza kusababisha jeshi ambalo lina nguvu na rasilimali, kujiona kama mbadala wa uongozi wa kiraia. Hivyo, badala ya kulinda katiba, linaweza kuamua kuingilia madaraka kwa madai ya kurejesha utulivu au haki.

Aidha, rushwa inapokithiri, inapunguza imani ya wananchi kwa serikali yao. Taasisi ya Transparency International imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa rushwa ni moja ya vichocheo vikuu vya kudhoofika kwa demokrasia na kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa.

Wananchi wanapohisi kuwa mifumo ya haki imevunjika na viongozi wanajinufaisha binafsi, huweza kuanza kuona mapinduzi ya kijeshi kama suluhisho, hata kama kwa muda mfupi.

Hii ni hali ya hatari, kwa kuwa mara nyingi mapinduzi hayo hayaishii kuleta mabadiliko ya kudumu, bali huanzisha mzunguko mpya wa migogoro.

Tamaa ya madaraka nacho ni kichocheo kingine kikubwa inatajwa kwa nchi nyingi za Afrika. Baadhi ya viongozi wa kijeshi huingia madarakani wakiahidi mageuzi, lakini baada ya muda hujikuta wakifuata nyayo za waliowaondoa.

Hali hii huendeleza mzunguko wa mapinduzi, kila kundi linaweza kutumia nguvu kuingia madarakani.

Kwa kuzingatia hali hiyo, ni wazi kuwa mapinduzi ya kijeshi barani Afrika yana tabia ya kujirudia kutokana na mchanganyiko wa sababu za ndani na nje. Bila kushughulikia mizizi ya tatizo, juhudi za kuyazuia zinaweza kuwa za muda mfupi tu.

Swali muhimu linabaki kuwa: je, mapinduzi haya yanaweza kuzuiwa?

Jibu ni ndiyo, lakini linahitaji hatua za kina na za muda mrefu. Inelezwa kwanza, ni lazima kuwe na juhudi za dhati za kuimarisha taasisi za kidemokrasia. Hii inahusisha kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, uhuru wa vyombo vya habari na mfumo wa mahakama unaojitegemea.

Pili, mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kupewa kipaumbele. Serikali zinapaswa kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji na kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote.

Tatu, ni muhimu kupunguza utegemezi wa kiuchumi unaochochea ukoloni mamboleo. Nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha uchumi wao wa ndani, kuongeza thamani ya rasilimali zao na kujenga ushirikiano wa kikanda unaolenga manufaa ya pamoja.

Pia, kuwe na uwekezaji katika elimu ya uraia na utamaduni wa demokrasia. Wachambuzi wanasema wananchi wanapaswa kuelewa haki na wajibu wao na kuona kuwa mabadiliko ya kisiasa yanaweza kupatikana kupitia njia za amani na kikatiba.

Kwa sababu ni muhimu kwa jumuiya za kikanda na kimataifa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.

Hata hivyo, inelezwa kuwa hatua hizi zinapaswa kuzingatia ushughulikiaji wa sababu zinazosababisha mapinduzi hayo badala ya kushughulikia matokeo pekee.

Na kwa kuwa mapinduzi ya kijeshi barani Afrika si tukio la bahati mbaya, inaelezwa ni matokeo ya mifumo yenye kasoro inayohusisha ukoloni mamboleo, rushwa, udikteta na tamaa ya madaraka.

Wachambuzi wanasema kama hatua madhubuti hazitachukuliwa kuyashughulikia matatizo haya kwa kina, mapinduzi hayo yataendelea kujirudia, kuwa sugu na kusababisha madhara makubwa kwa maendeleo ya bara hili.

Hivyo, ni wakati sasa kwa viongozi, wananchi na wadau wa maendeleo kushirikiana kujenga mifumo imara inayozuia mapinduzi ya kijeshi na kuimarisha utawala wa sheria, demokrasia na maendeleo jumuishi kwa mustakabali wa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *