
Dini zote zinatufundisha kuwa na moyo wa shukrani kwa kila hatua njema, hata kama ni ndogo, ili kufungua njia ya mafanikio makubwa zaidi.
Kwa msingi huo, ni vyema kuanza kwa kutoa pongezi na shukrani kwa Jaji Chande pamoja na timu yake kwa kukamilisha na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu ya Oktoba 29. Kitendo cha kuandaa na kuweka hadharani taarifa hii ni hatua muhimu katika kutafuta ukweli na haki.
Hata hivyo, pamoja na mchango huo, ni wazi kuwa ripoti hiyo haijakidhi kikamilifu matarajio ya Watanzania wengi waliokuwa na kiu ya kuona haki inatendeka kwa uwazi na ukamilifu. Mojawapo ya mambo yaliyobainishwa ni idadi ya watu 518 waliopoteza maisha katika vurugu hizo.
Idadi hii ni kubwa sana na haiwezi kuchukuliwa kama matokeo ya bahati mbaya au ajali za kawaida.
Ripoti inaonesha kuwa sehemu kubwa ya vifo hivyo vilitokana na matumizi ya risasi za moto. Hata hivyo, haijaweka wazi ni nani aliyetoa amri ya kutumia nguvu hiyo kubwa dhidi ya raia, wakiwamo waandamanaji ambao wengi wao hawakuwa na silaha za moto.
Kwa mantiki ya kiusalama na kitaaluma, kulikuwa na njia mbadala za kudhibiti ghasia bila kufikia hatua ya kuua, kama vile kutumia nguvu isiyo ya kuua au kulenga sehemu zisizo hatari mwilini.
Zaidi ya hapo, ukosefu wa taarifa kuhusu hatua za uwajibikaji dhidi ya vifo hivyo unazua maswali mazito. Historia ya nchi yetu inaonesha mifano ya uwajibikaji madhubuti pale matukio kama haya yalipotokea.
Mwaka 1976 baada ya vifo vya mahabusu wachache tu mikononi mwa vyombo vya dola katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, hatua kali zilichukuliwa dhidi ya viongozi wa juu serikalini na vyombo vya usalama. Hii inaonesha kuwa uwajibikaji si jambo jipya katika utawala bora.
Kwa kuzingatia hilo, ni halali kujiuliza: ni idadi gani ya vifo inahitajika ili hatua za uwajibikaji zichukuliwe leo? Viongozi wa juu wa vyombo vya ulinzi na usalama bado wako madarakani bila maelezo ya kina kuhusu jukumu lao katika matukio haya.
Katika mfumo wa “chain of command,” ni wazi kuwa uamuzi mkubwa kama huu hauwezi kufanyika bila maelekezo kutoka ngazi za juu. Ripoti pia imeonesha kuwa baadhi ya waliouawa hawakuwa waandamanaji, bali ni raia wa kawaida, wakiwamo watoto wadogo wasio na hatia.
Hili linaongeza uzito wa hoja kwamba matumizi ya nguvu hayakuwa ya uwiano wala ya lazima katika baadhi ya mazingira. Ushahidi wa picha, video na mashuhuda unaimarisha hoja hii.
Pamoja na hayo, ni muhimu kutambua kuwa ripoti imechukua hatua ya wazi kwa kutangaza idadi rasmi ya vifo. Hii ni ishara ya uwazi na ujasiri, na inapaswa kuungwa mkono.
Hata hivyo, ili kuimarisha imani ya umma, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa familia za wahanga zinapata taarifa kamili, ikiwamo majina ya marehemu na maeneo walipozikwa.
Hatua hii itasaidia kuondoa sintofahamu na uvumi uliokuwapo kuhusu uwepo wa makaburi ya halaiki.
Baada ya kupatikana kwa taarifa hizi, kuna haja ya serikali kuchukua hatua kadhaa muhimu. Kwanza, kuweka wazi nani alitoa amri ya kutumia risasi za moto.
Uwajibikaji wa wazi ni msingi wa haki na utawala bora. Pili, kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya wahusika, kama ilivyowahi kufanyika katika historia ya nchi yetu.
Tatu, serikali inapaswa kushughulikia taarifa potofu zilizoripotiwa kimataifa kuhusu idadi ya vifo. Ni kweli kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya nje vilitoa takwimu zinazokinzana na ripoti rasmi.
Hata hivyo, njia bora ya kukabiliana na hali hiyo ni kupitia diplomasia makini na utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati, badala ya kuingia kwenye mvutano usio wa lazima.
Nne, ni muhimu kwa serikali kushirikiana na wataalamu wa sheria wa ndani na kimataifa ili kulinda taswira ya nchi, lakini pia kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wahanga.
Hii inapaswa kufanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.
Mwisho, serikali inapaswa kutoa tamko rasmi linaloeleza ukweli wa tukio hili, ili kuondoa mkanganyiko uliopo ndani na nje ya nchi.
Ukimya unaweza kutoa nafasi kwa taarifa zisizo sahihi kuendelea kuaminika kama ukweli.
Kwa ujumla, ripoti ya Jaji Chande ni hatua muhimu, lakini si mwisho wa safari ya haki. Watanzania wanahitaji kuona hatua za vitendo zikichukuliwa.
Hivyo basi, hatupaswi kusubiri wala kunyamaza, ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha haki inatendeka na inadhihirika.