Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kuonekana kwenye pasipoti mpya maalumu zitakazotolewa kuadhimisha miaka 250 tangu kupatikana kwa uhuru wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa Fox News na Al Jazeera maofisa wa serikali wamesema pasipoti hizo za kumbukumbu zitakuwa na picha ya Trump pamoja na saini yake, ikiwa ni sehemu ya muundo mpya unaojumuisha vipengele vya kihistoria kama maandishi ya Declaration of Independence na bendera ya Marekani.

Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 250 ya Azimio la Uhuru wa Marekani wa mwaka 1776, ambapo matukio mbalimbali ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika kote nchini ikiwemo mbio za magari.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tommy Pigott amesema pasipoti hizo zitatolewa kwa idadi maalumu na zitapatikana kwa raia wa Marekani watakaoomba kupitia ofisi ya pasipoti ya Washington wakati wa uzinduzi msimu huu wa kiangazi.

Kwa sasa, pasipoti za kawaida za Marekani huonyesha picha na alama za kihistoria zinazohusiana na utambulisho wa taifa hilo, ikiwemo tukio la vita vya Fort McHenry lililomhamasisha Francis Scott Key kuandika wimbo ambao kwa sasa ndiyo wa taifa Marekani.

Kurasa nyingine za pasipoti hizo pia huonyesha matukio muhimu kama kutua chombo cha anga cha Apollo 11 Moon Landing pamoja na alama maarufu kama Sanamu ya Uhuru (Statue of Liberty).

Hata hivyo, uamuzi wa kuweka picha ya Rais wa sasa kwenye hati rasmi ya kusafiria umeibua mjadala. Wapo wanaounga mkono wakisema ni njia ya kuimarisha uzalendo na kuenzi uongozi, huku wakosoaji wakidai kuwa hatua hiyo inaingiza siasa katika nyaraka za kitaifa.

Ripoti zinaeleza mpango huo ni sehemu ya juhudi pana za utawala wa Trump kuweka alama yake katika taasisi mbalimbali za serikali. Tayari, baadhi ya miradi mingine imehusisha kuweka picha yake kwenye nyaraka za kuingilia hifadhi za taifa na hata mapendekezo ya sarafu mpya yenye sura yake.

Licha ya maandalizi hayo, mjadala unaendelea kuhusu iwapo hatua hiyo inafaa katika kuenzi historia ya taifa au ni sehemu ya kujenga taswira ya kisiasa ya kiongozi aliyepo madarakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *