
Wafanyakazi duniani wanatarajiwa kuadhimisha Siku yao ya kimataifa ya Wafanyakazi maarufu kwa jina la Mei Mosi, keshokutwa Ijumaa.
Siku ambayo hugeuka kuwa fursa muhimu ya kutafakari hali ya mazingira ya kazi, haki na maslahi yao wakiwa kazini na hata wanapostaafu.
Siku hii yenye chimbuko lake nchini Marekani mwaka 1886, iliashiria mwanzo wa harakati za wafanyakazi kudai haki zao, hususan kupunguza saa za kazi na kuboresha mazingira ya ajira. Tangu wakati huo, imeendelea kuwa alama ya mshikamano wa wafanyakazi duniani kote.
Kwa muktadha huo, Mei Mosi ni wakati mwafaka kwa wafanyakazi kutathmini mafanikio yao, kubaini changamoto wanazokumbana nazo na kuimarisha mshikamano katika kudai haki zao.
Miongoni mwa madai ya msingi ya kihistoria ni pamoja na kupunguza muda wa kazi usizidi saa nane kwa siku, kuboresha mishahara na kuhakikisha mazingira salama ya kazi.
Visiwani Zanzibar, maadhimisho ya kwanza ya Mei Mosi yalifanyika mwaka 1964, miezi michache baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Hata hivyo, harakati za wafanyakazi zilianza mapema zaidi, hasa katikati ya miaka ya 1940, zikichochewa na mazingira magumu ya kazi hususan katika sekta ya bandari.
Mwaka 1948, Zanzibar ilishuhudia mgomo mkubwa wa wafanyakazi wa bandarini uliosababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi kwa zaidi ya wiki moja.
Mgomo huo uliathiri si tu Zanzibar, bali pia nchi jirani, baada ya meli kushindwa kupakia na kupakua mizigo. Serikali ililazimika kuleta wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja, lakini jitihada hizo zilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa waliokuwa katika mgomo.
Matokeo ya mgomo huo yalikuwa na manufaa makubwa kwa wafanyakazi. Walifanikiwa kupata mkataba uliopunguza saa za kazi kutoka tisa hadi nane kwa siku, pamoja na kupata huduma muhimu kama chakula na matibabu kutoka kwa waajiri.
Aidha, mgomo huo uliweka msingi wa kuanzishwa kwa vyama vya wafanyakazi, ambavyo baadaye vilihusishwa kwa karibu na vyama vya siasa.
Baadhi ya viongozi wa harakati hizo, akiwamo Abeid Amani Karume, walihusika pia katika kuunda vyama vya siasa vilivyoongoza harakati za ukombozi.
Wengine ni pamoja na Jamal Ramadhani Nasibu, Hassan Nassor Moyo na Badaway Qulatein, waliokuja kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Baada ya mapinduzi ya 1964, kulisikika nyimbo na kaulimbiu zilizotukuza heshima ya wafanyakazi na wakulima, zikiwahamasisha kushiriki katika ujenzi wa taifa jipya lenye usawa na haki. Hata hivyo, pamoja na historia hiyo ya harakati na mafanikio, hali ya wafanyakazi Zanzibar leo inaibua maswali mengi. Licha ya kuwapo kwa vyama vya wafanyakazi katika sekta mbalimbali, sauti zao hazisikiki ipasavyo isipokuwa wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi.
Kwa sasa, kuna malalamiko mengi ya unyanyasaji, udhalilishaji na uonevu wa wafanyakazi, hasa katika sekta binafsi kama hoteli na baa.
Wafanyakazi wengi wanakabiliwa na mazingira magumu ya kazi, hulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko ya kutosha na kulipwa mishahara midogo isiyokidhi hata viwango vya chini vilivyowekwa na serikali.
Katika baadhi ya maeneo ya kazi, wafanyakazi hawana mikataba rasmi, hali inayowafanya wawe katika hatari ya kufukuzwa kazi wakati wowote bila utaratibu. Wapo wanaolipwa chini ya Sh100,000 kwa mwezi, huku wengine wakiona siku ya mapumziko kama bahati adimu.
Aidha, kuna tuhuma nzito kuhusu ukiukwaji wa maadili katika baadhi ya baa, ambapo wafanyakazi hulazimika kulipa fedha ili kuondoka mapema kazini au kushinikizwa kuvaa mavazi yasiyoendana na utu wao ili kuwavutia wateja.
Vitendo hivi vinakiuka haki za binadamu na vinapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Inasikitisha pia kwamba vyama vya wafanyakazi vinaonekana kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulinda maslahi ya wanachama wao. Wafanyakazi wengi wanasema hawajawahi kutembelewa na viongozi wa vyama hivyo wala kufanyiwa ukaguzi wa mazingira ya kazi.
Kwa upande mwingine, Idara ya Kazi ya serikali imekuwa ikilaumiwa kwa kutofuatilia ipasavyo malalamiko ya wafanyakazi. Baadhi ya wafanyakazi wanasema wanapowasilisha malalamiko yao, hupata majibu yasiyoridhisha na hakuna hatua za haraka zinazochukuliwa.
Serikali ina wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi sambamba na kuvutia uwekezaji. Ni muhimu kuhakikisha kuwa jitihada za kuvutia wawekezaji hazifanywi kwa gharama ya kudhalilisha utu na haki za wafanyakazi.
Aidha, changamoto hazipo tu katika sekta binafsi, bali pia ndani ya taasisi za serikali, ambako baadhi ya viongozi huwanyanyasa watumishi walio chini yao, huku wengine wakikosa uwajibikaji kazini.
Kwa ujumla, Zanzibar ina sheria zinazolenga kulinda haki za wafanyakazi na waajiri. Hata hivyo, utekelezaji wake unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha haki hizo zinazingatiwa kwa vitendo. Wakati huo huo, wafanyakazi nao wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa uadilifu na bidii.