Baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 wakati wa uchaguzi mkuu, Watanzania wengi walijikuta katika hali ya sintofahamu, migawanyiko ya kisiasa na kupungua kwa imani miongoni mwa wananchi.

Hata hivyo, ukidadisi, hali hii si ya kipekee kwa Tanzania, bali ni changamoto inayoweza kujitokeza kwa wananchi wa nchi yoyote ile duniani inayopitia mchakato wa kisiasa wenye ushindani mkali.

Lakini huenda kwa Tanzania ikawa tofauti kwa sababu historia yake imejengwa juu ya misingi ya umoja, mshikamano na amani, nguzo ambazo ni muhimu kurejeshwa kwa njia ya maridhiano ya kweli na ya kudumu pindi zinapotetereka kama wasemavyo wachambuzi wa masuala ya siasa duniani.

Wanasema njia bora ya kwanza katika kufanikisha maridhiano ni kuwapo kwa majadiliano ya wazi na jumuishi.

Njia hii inaelezwa kwamba inahitaji viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii kukaa pamoja na kujadili kwa uwazi yale yaliyotokea bila woga au upendeleo.

Majadiliano haya yanapaswa kulenga ukweli, si lawama. Pale ambapo ukweli unakubaliwa na pande zote, inakuwa rahisi kujenga msingi wa kuelewana na kusonga mbele kama taifa moja.

Pili, ni muhimu kuimarisha taasisi za haki na uwajibikaji. Wananchi wanapopoteza imani katika mifumo ya haki, huanza kujenga hisia za kukata tamaa na hasira.

Serikali na vyombo husika vinapaswa kuhakikisha kuwa malalamiko yote yanayohusiana na uchaguzi yanachunguzwa kwa haki na hatua stahiki kuchukuliwa bila upendeleo. Hii itasaidia kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi zao na kupunguza uwezekano wa migogoro ya baadaye.

Elimu ya uraia pia ni nguzo muhimu katika kujenga maridhiano ya kudumu. Wananchi wanahitaji kufahamu haki zao, wajibu wao na umuhimu wa kuheshimu mitazamo tofauti. Elimu hii inaweza kutolewa kupitia vyombo vya habari, shule na mikutano ya kijamii.

Wananchi wanaotambua umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimu tofauti, mara zote huwa na uwezo mkubwa wa kushinda changamoto za kisiasa bila kuvunjika.

Aidha, jukumu la vyombo vya habari haliwezi kupuuzwa. Katika nyakati za mvutano wa kisiasa, tunaambiwa kuwa vyombo vya habari vinayo nafasi kubwa ya kuchochea au kupunguza migogoro.

Hivyo mi muhimu kwa vyombo hivi kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kutoa taarifa sahihi, zisizo na upendeleo na zinazochochea amani badala ya chuki. Lugha inayotumiwa katika kuripoti matukio inapaswa kuwa ya kujenga na kuhamasisha mshikamano wa kitaifa.

Na tunaambiwa kwamba viongozi wa dini nao wanayo nafasi ya kipekee katika kuhamasisha maridhiano.

Kila mmoja anafahamu kwamba Tanzania ni taifa lenye watu wa imani tofauti na viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii. Hivyo, kwa kutumia majukwaa yao, wanaweza kuhubiri amani, msamaha na upendo, wakikumbusha waumini wao kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuvunja uhusiano wa kijamii na kibinadamu.

Kwa sababu maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana bila watu kuwa tayari kusamehe na kusahau maumivu ya nyuma.

Nasema hivyo kwa sababu hii haimaanishi kupuuza haki, bali ni hatua ya kujenga upya uhusiano uliovunjika. Tukumbuke kwamba hatua kama hizi mara zote hulenga kuwaleta watu pamoja kutoka makundi tofauti na zinaweza kusaidia sana katika mchakato kama huu wa kuyaendea maridhiano ambao nchi unautazama.

Na katika hatua hii, ni wazi kuwa vijana wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika juhudi zote za kuleta maridhiano.

Kwa sababu mara nyingi vijana ndio wanaobeba athari kubwa za migogoro ya kisiasa, lakini pia wana uwezo mkubwa wa kuwa sehemu ya suluhisho.

Hivyo kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mijadala, miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii, wanaweza kuwa daraja la kuunganisha jamii na kuleta mabadiliko chanya.

Kwa maana nyingine, nadiriki kusema maridhiano si tukio la mara moja bali ni mchakato endelevu unaohitaji dhamira ya kweli kutoka kwa kila Mtanzania.

Na kwa kupitia majadiliano ya wazi, kuimarisha taasisi za haki, elimu ya uraia, uwajibikaji wa vyombo vya habari, mchango wa viongozi wa dini, utamaduni wa msamaha na ushiriki wa vijana, Tanzania inaweza kurejea katika misingi yake ya umoja na mshikamano.

Kwa hiyo, ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa tofauti za kisiasa hazigeuki kuwa chanzo cha migawanyiko ya kudumu, bali zinakuwa fursa ya kujenga taifa imara zaidi lenye kuheshimu utofauti wake.

Lilian Timbuka ni Mhariri wa habari za siasa sambamba na jarida lake ndani ya Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *