
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua awamu ya pili ya kupokea mawazo bunifu kutoka kwa umma kwa lengo la kuongeza wigo wa kodi na kuboresha huduma, ikitaja vipaumbele sita.
Vipaumbele hivyo ni upanuzi wa wigo wa kodi, hususan katika sekta isiyo rasmi; maboresho ya ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo; uboreshaji wa huduma za kidijitali na usimamizi wa kodi matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa kodi; uboreshaji wa utatuzi wa migogoro ya kikodi; na njia za kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa wananchi.
Katika awamu ya pili, TRA pia imefanya maboresho kadhaa, ikiwamo kutojihusisha moja kwa moja katika maamuzi ya tathmini ya mawazo. Badala yake, imeunda kamati huru ya watu 12 inayojumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali ili kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Aprili 29, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema awamu hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi na kujenga imani kwa kuwapa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa mawazo bunifu ya kuongeza wigo wa kodi.
Akieleza mchakato wa awamu ya kwanza, Mwenda amesema wananchi 5,681 waliwasilisha mawazo yao, ambapo mawazo 106 yaliingia katika hatua ya tathmini ya kina na hatimaye mawazo tisa kuchaguliwa kuwa bora.
“Mawazo yote yaliyoshinda hayajapotea, tunaendelea kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wabunifu ili yaweze kusaidia kuboresha utendaji wa TRA,” amesema Mwenda.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza, ikiwemo mfumo kutokuwa wazi vya kutosha na mchakato wa tathmini kukosa uhuru wa kutosha, Mwenda amesema zimefanyiwa kazi ili kuhakikisha awamu ya pili inakuwa huru, wazi na yenye kuaminika zaidi.
Kwa mujibu wa Mwenda, katika awamu hii TRA haitashiriki moja kwa moja katika maamuzi ya tathmini ya mawazo, bali imeunda kamati huru inayojumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali ili kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa.
Vipaumbele sita
Akitoa ufafanuzi wa maeneo ya kipaumbele, Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa TRA, Ephraim Mdee, amesema mawazo bunifu yatapaswa kulenga upanuzi wa wigo wa kodi, hususan katika sekta isiyo rasmi; maboresho ya ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo; na uboreshaji wa huduma za kidijitali na usimamizi wa kodi.
Vingine ni matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa kodi, uboreshaji wa utatuzi wa migogoro ya kikodi na njia za kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa wananchi.
Amesema mfumo mpya wa kupokea mawazo umeboreshwa na kuwa wa kielektroniki, ambapo mshiriki ataweza kufuatilia hatua zote za mchakato tangu kuwasilisha wazo lake hadi hatua ya tathmini.
“Katika tathmini, tutaangalia uhalisia wa wazo, mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali, uwezo wa kuboresha huduma kwa walipa kodi pamoja na ubunifu wake,” amesema Dk Mdee.
Namna ya kushiriki
Akieleza utaratibu wa kushiriki, mchumi kutoka Idara ya Utafiti na Mipango TRA, Hidaya Maduhu, amesema mchakato unafanyika kwa njia ya kidijitali kupitia tovuti ya TRA.
Amesema mshiriki anapaswa kuingia kwenye tovuti rasmi ya TRA kisha kuchagua sehemu ya Innovation, ambapo atasajili akaunti kwa kutumia namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) na nenosiri. Baada ya kujaza taarifa hizo, mfumo utafunguka na kumpa nafasi ya kuanza kuwasilisha wazo.
“Mshiriki anaweza kujisajili kama mtu binafsi au kama kikundi, kisha akaanza kujaza taarifa za wazo bunifu,” amesema Maduhu.
Katika hatua ya uwasilishaji, mshiriki anatakiwa kuandika kichwa cha wazo (title), kubainisha kama ni wazo jipya, na kutoa maelezo ya kina yanayoeleza wazo hilo linahusu nini na namna litakavyotekelezwa, maeneo ambayo litaleta matokeo chanya, pamoja na kuchagua aina ya athari anayolenga katika mfumo wa kodi au huduma za TRA.
Kwa mujibu wa Maduhu, ni muhimu pia kueleza rasilimali zitakazohitajika ili kutekeleza wazo husika, jambo litakalosaidia katika tathmini ya utekelezaji wake. Mshiriki atapaswa pia kuambatanisha nyaraka za ziada katika mfumo wa PDF, kisha kuwasilisha wazo lake.
“Baada ya kuwasilisha, mfumo utakuwa ukimpa mrejesho wa hatua aliyofikia, na pia atakuwa na nafasi ya kuwasilisha mawazo zaidi ya moja,” amesema.
Naye Makamu wa Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara, Boniface Ndego, amesema mpango huo utaongeza tija kwa kuwa unahusisha wadau wote na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wananchi.
Amesema ushirikishwaji utasaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Zawadi zaboreshwa
Tofauti na awamu ya kwanza, msimu huu TRA imeboresha zawadi ambapo nafasi ya pili na ya tatu zitakuwa na washindi wanne, huku nafasi ya nne ikiwa na washindi 15.
Mwenda amesema mshindi wa kwanza ataondoka na Sh50 milioni, wakati watu wawili watakaoshika nafasi ya pili kila mmoja atazawadiwa Sh30 milioni. Vivyo hivyo kwa washindi wawili wa nafasi ya tatu ambao kila mmoja ataondoka na Sh20 milioni.
“Awamu ya kwanza tulitoa zawadi kwa washindi tisa; awamu hii tunatoa kwa washindi 20. Hivyo, watu 15 watakaofuata wote watakuwa wamekamata nafasi ya nne, kila mmoja atazawadiwa Sh10 milioni,” amesema Mwenda.
Mbali na watu hao 20 watakaoongoza, Mwenda amesema wale wote watakaoingia hatua ya tathmini bila kujali idadi yao, kila mmoja atapewa Sh100,000.
Awali, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan amesema mawazo yatakayowasilishwa yanapaswa kuonyesha teknolojia itakavyotumika katika ukusanyaji wa kodi, namna ya kuwafikia walipa kodi wote na mbinu za kuwafanya wananchi walipe kodi kwa hiari.
Amesema awamu ya pili ya shindano hilo inatarajiwa kuongeza ubunifu unaotekelezeka na wenye athari ya moja kwa moja katika kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha huduma za TRA kwa wananchi.