
Tangu kuanza kwa mashambulizi makali ya pamoja kati ya Israel na Marekani nchini Iran miezi miwili iliyopita, takriban watu 21 wamenyongwa na maelfu ya wengine kukamatwa.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari ilyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, Türk ameeleza kushtushwa kwake na hali hiyo akisema, “Nimeshtushwa kwamba pamoja na athari mbaya za mzozo zinazoshuhudiwa, haki za watu wa Iran zinaendelea kupokonywa kutoka kwao na mamlaka, kwa njia kali na za kikatili.”
Hukumu za kunyongwa
Ripoti zinaonesha kuwa miongoni mwa walionyongwa, tisa walihusishwa na maandamano ya Januari 2026, kumi kwa madai ya uanachama katika makundi ya upinzani, na wawili kwa mashtaka ya ujasusi. Türk amesisitiza kuwa hata katika nyakati za vita, haki za msingi lazima zilindwe.
“Katika nyakati za vita, vitisho dhidi ya haki za binadamu huongezeka kwa kasi kubwa. Hata hivyo, hata pale usalama wa taifa unapotajwa, haki za binadamu zinaweza tu kuwekewa mipaka pale ambapo ni lazima kabisa na kwa adhabu inayolingana na kosa, na kwa lengo halali. Na haki za msingi, zisizoweza kuingiliwa kama vile ulinzi dhidi ya kuzuiliwa kiholela, na haki ya kesi kusikilizwa kwa haki lazima ziheshimiwe kikamilifu, wakati wote,” amesema Volker Türk.
Hali ya magereza nchini Iran inatisha
Hali ya magereza nchini Iran imetajwa kuwa ya kutisha, ambapo wafungwa wanateseka kwa msongamano mkubwa na ukosefu wa mahitaji muhimu. Türk ametoa wito wa dharura kwa kusema, “Natoa wito kwa mamlaka kusitisha hukumu zote za kunyonga zilizopangwa, kusitisha matumizi ya adhabu ya kifo, kuhakikisha kikamilifu mchakato unaostahili na dhamana kwa kesi zenye haki hiyo, na kuwaachilia mara moja wale waliozuiliwa kiholela.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Iran watu wengi wakiwemo watoto wanasalia katika hatari ya adhabu ya kifo. Washtakiwa hao mara nyingi wanakabiliwa na kesi zinazoendeshwa haraka mahakamani na kunyimwa msaada wa mawakili binafsi wa kisheria.
Matumizi ya mateso na unyanyasaji pia yameripotiwa mara kwa mara. Baadhi ya hukumu za mahakama zilizotolewa dhidi ya waandamanaji wakiwemo takribani tisa walionyongwa ziliripotiwa kuwa zilitokana na kukiri kosa kwa kulazimishwa.
Tangu Februari 28 mwaka huu, zaidi ya watu 4,000 wanakadiriwa kukamatwa kwa mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa nchini Iran.
Wafungwa wengi wametoweshwa kwa nguvu, kuteswa, au kutendewa aina nyingine za ukatili, unyama na udhalilishaji. Watu kutoka makabila madogo na kidini, ikiwa ni pamoja na Bahá’ís, Zoroastrians, Kurds, na Baluch Iranians, wamekuwa katika hatari kubwa. Makumi ya wafungwa wamehamishiwa maeneo yasiyojulikana bila taarifa yoyote kuhusu hatima yao, miongoni mwao ni wakili wa haki za binadamu Nasrin Sotoudeh.
“Hali za watu walio kizuizini katika magereza ya Iran ni mbaya. Wafungwa wanateseka kutokana na msongamano mkubwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji, vifaa vya usafi, dawa na wananyimwa huduma ya matibabu,” ameeleza Volker Türk.
Afya ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Narges Mohammadi, ambaye bado ameshikiliwa pamoja na wahalifu wa vurugu, inaripotiwa kuwa mbaya zaidi baada ya kupata mshtuko wa moyo.
Hali yake ya kiafya pia inachangiwa na hali mbaya za kiafya zinazotokana na kukamatwa kwake.
Katika Gereza la Chabahar, wafungwa waliopinga kusimamishwa kwa muda mrefu kwa usambazaji wa chakula, walipigwa. Vikosi vya usalama vimeripotiwa kuwaua takriban watano na kujeruhi 21 baada ya kukabiliana na waandamanaji. Wafungwa wawili walifariki wakiwa kizuizini, katika gereza tofauti, na kuashiria kuwa walikuwa wameteswa.
Teknolojia yatumika kuzima mtandao na kutaifisha mali
Mbali na ukandamizaji wa kimwili, serikali imetumia teknolojia kudhibiti raia kwa kukata mtandao kwa siku 61 mfululizo na kutaifisha mali za raia wapatao 675, wakiwemo 400 wanaoishi nje ya nchi, miongoni mwao ni waigizaji, wanariadha, watumishi na waandishi wa habari wakiwataja kuwa wasaliti kwa ardhi ya nyumbani wakiwashutumu kwa kuunga mkono mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Türk ameonya kuwa “Hii inawanyima watu kote nchini upatikanaji wa habari muhimu, kunyamazisha sauti huru, na kusababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi. Tayari imezidisha hali mbaya ya kibinadamu na kiuchumi, na lazima iondolewe mara moja.”