
ACHA wauane. Ndivyo unavyoweza kuelezea kufuatia tambo za makocha wa Mbeya City, Salum Mayanga na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wa Mashujaa katika vita ya pointi tatu za mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mchezo huo ambao utapigwa kesho Alhamisi, unatarajia kuwa na upinzani kutokana na matokeo ya timu zote Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo wenyeji Mbeya City wapo nafasi ya 14 kwa pointi 17, huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 11 kwa pointi 21.
Timu hizo zinakutana ikiwa Mashujaa haijapata ushindi katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu, ikiambulia sare pekee, huku Mbeya City ikikumbuka kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga ambacho kilihitimisha safari ya Kocha Mecky Maxime, ndipo Mayanga atachukua nafasi yake.
Utamu wa mechi hiyo unakumbusha tukio la Mashujaa kuishusha Mbeya City msimu wa 2022-2023 walipokutana play pff kwenye Uwanja wa Sokoine na kuwalaza bao 1-0, huku mechi ya mwisho kukutana mkoani Kigoma msimu huu, Mbeya City ilikufa bao 1-0.
Mayanga ambaye utakuwa mchezo wake wa kwanza kuiongoza Mbeya City tangu atambulishwe kikosini hapo, amesema wanafahamu ugumu na umuhimu wa mechi hiyo, akieleza kuwa maandalizi waliyofanya anaamini watashinda.
Amesema wachezaji wameonesha ari na morali katika mazoezi yao akifafanua kuwa wapo katika mazingira magumu, hivyo jambo moja kwao ni kushinda mchezo huo ili kufufua na kurejesha matumaini mapya.
“Wachezaji waliokuwa majeruhi wamerejea, muda niliokaa na timu nimerekebisha makosa, tunajua ugumu wa wapinzani ila tunalohitaji ni pointi tatu ili kurejesha matumaini mapya kikosini,” amesema Mayanga.
Kwa upande wake nahodha na straika wa timu hiyo, Eliud Ambokile, amesema kwa sasa hawafikirii zaidi matokeo ya mechi zilizopita badala yake yaliyotokea wamesahau na sasa akili ni mchezo wa kesho.
“Ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa timu zote na uhitaji wa pointi, wachezaji tuko tayari kupambania pointi tatu, tunaomba mashabiki waje kwa wingi kutusapoti,” amesema straika huyo.
Naye Julio amesema kwa sasa ligi haina cha ugenini wala nyumbani akiwapongeza baadhi ya waamuzi kwa kuchezesha vyema na kwamba kiu yao ni kupata pointi tatu.
Kuhusu mwenendo wa timu hiyo, kocha huyo amesema tangu ametua kikosini amefanya mabadiliko mengi na hajapoteza mchezo wowote, jukumu lililobaki ni la wachezaji kufunga.
“Nimerekebisha mengi ikiwamo morali, kutengeneza nafasi na sasa kazi iliyobaki ni utulivu wa mchezaji mwenyewe kufunga mabao, naendelea kutengeneza timu na mafanikio yapo kwakuwa sijapoteza mechi,” amesema Julio.