KOCHA wa Simba, Steve Barker amewataka mastaa wake kuachana na sherehe za ubingwa wa Muungano walilotwaa juzi Jumatano huko Zanzibar baada ya kuichapa Yanga na  badala yake waelekeze nguvu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Jumapili hii dhidi ya wapinzani wao wa jadi.

Bao la Seleman Mwalimu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 118, lilitosha kuifanya Simba kumaliza uteja kwa Yanga baada ya kupoteza mechi sita kati ya saba za mwisho katika mashindano yote kabla ya ushindi huo.

Kocha huyo amesema ushindi huo ulikuwa muhimu kwa morali ya timu lakini haupaswi kuwafanya wachezaji wake kupoteza umakini katika malengo makubwa ya msimu huu.

Barker amesema ubingwa huo ni sehemu ya safari, sio mwisho wa kazi, hivyo nidhamu lazima iendelee kuwa juu katika kikosi chake.

PUM 06

Raia huyo wa Afrika Kusini, amesema kwa sasa Simba inaelekeza nguvu zote katika maandalizi ya mechi dhidi ya Yanga, ambayo anaitaja ni moja ya mechi ngumu na yenye presha kubwa.

“Tumefurahia Kombe la Muungano na tulipata upinzani mkubwa kutoka kwa Yanga, nikiri wana timu nzuri lakini ya Zanzibar yamepita, sasa akili zetu ziko kwenye mchezo unaofuata ambao kimsingi utakuwa tofauti kabisa,” amesema na kuongeza;

“Kwetu hii itakuwa nafasi ya kuonyesha zaidi nini tunaweza kufanya, tukiwa katika uwanja wa mazoezi tutaboresha mapungufu ambayo yalionekana katika fainali ya Zanzibar.”

PUM 05

Mechi hiyo ya ligi  inakuja ikiwa na uzito mkubwa kutokana na hali ya msimamo wa inayoendelea kushika kasi na Yanga inaongoza na pointi 47 baada ya kucheza mechi 19, ikiwa na mwenendo mzuri msimu huu. Simba wapo nafasi ya pili na pointi 42, tofauti ya pointi tano ikiwaweka katika mazingira ya kupambana zaidi ili kupunguza pengo hilo.

Barker amesema tofauti hiyo ya pointi haibadilishi malengo ya Simba, bali inaongeza hamasa ya kupigania matokeo mazuri katika kila mchezo.

Ameongeza, mechi za aina ya dabi huwa hazitabiriki na mara nyingi huamuliwa na makosa madogo na umakini wa dakika zote 90.

PUM 04

Kocha huyo amesema kwa muda mchache ambao umesalia, amelenga kufanya maboresho katika eneo la umaliziaji pamoja na uimara wa ulinzi.

Alieleza wachezaji wake wanaelewa ukubwa wa mchezo huo na tayari wako katika hali nzuri ya kiakili na kimwili.

SIMBA YARUDI DAR, YANGA YABAKI

Wakati huohuo, mabosi wa Simba wamefanya uamuzi wa haraka kuiwahisha timu Dar es Salaam ili kufanya maandalizi ya mechi ya Jumapili na wao watakuwa wenyeji.

Katika uamuzi huo, mara tu baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Muungano kumalizika sambamba na sherehe zote za kukabidhiwa kombe kufanyika, baadhi ya wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo walirejea Dar fasta kwa usafiri wa ndege, huku wengine wakirejea na boti.

PUM 03

Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizipata kutoka Simba, wameamua kufanya hivyo ili kupata muda mzuri zaidi wa kujiandaa kwani bado wana uhitaji wa kushinda mechi hiyo nyingine.

“Wachezaji ambao walianza katika mechi dhidi ya Yanga, waliondoka mapema kwa ndege kurejea Dar es Salaam wakiwa na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi, kisha wale ambao hawakupata muda mwingi wa kucheza au ambao hawakucheza kabisa, walirejea na boti wakiwa na kombe.

“Tumefanya hivyo ili kuwawahisha wachezaji kuja kupumzika, kisha kuanza mara moja maandalizi ya mechi ya Jumapili ambayo pia bado tunahitaji ushindi,” amesema kiongozi mmoja wa Simba.

PUM 02

Wakati Simba ikirudi fasta Dar, kikosi cha Yanga kimesalia Zanzibar kikiendelea na maandalizi ya mechi hiyo ya Jumapili. Kiongozi mmoja wa Yanga aliliambia Mwanaspoti, uamuzi huo umefanyika ili kuweka utulivu ndani ya kikosi baada ya kupoteza dabi ya kwanza kwani hawataki ijirudie kwenye ligi.

“Timu itaendelea kuwepo Zanzibar na tunatarajia kwenda Dar siku ya mechi, tumeamua kufanya hivyo ili kuweka utulivu kwenye timu huku hesabu zikiwa ni kushinda mechi ya Jumapili na kuendelea kujitanua kileleni mwa msimamo wa ligi,” amesema bosi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *