Arusha. Mabaki ya miili ya watu watatu wa familia moja waliofariki kwa ajali ya moto,inatarajiwa kuzikwa kesho Mesi Mosi, 2026 katika Kijiji cha Msangeni,Ugweno wilayani Mwanga, Kilimanjaro.
Alfajiri ya Jumanne Aprili 28,2026, watu watatu ambao ni bibi na wajukuu zake wawili, Mkunde Ephata (85) na wajukuu zake wawili, Jackson Geofrey (26) na Lerato Shabani (11), walifariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kutetekea kwa moto.
Nyumba hiyo iliyopo Kijiji cha Mjimwema,Kata ya Usa River,wilayani Arumeru iliteketea kwa moto ambao hadi sasa chanzo chake hakijajulikana,ulitokea alfajiri ya jana kijijini hapo na kusababisha vifo vya watu hao wa familia moja.
Tofauti na ilivyozoeleka katika misiba mingine,kutokana na nyumba hiyo kuungua na kuisha yote,wanafamilia wa bibi na wajukuu hao wamelazimika kufunga hema kubwa mbili nje ya nyumba hiyo na lingine katika uwanja uliopo jirani nao,kuendelea kuomboleza.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Aprili 30, 2026 nyumbani hapo, msemaji wa familia hiyo, Kitia Wilderson,amesema kuwa wanatarajia kuchukua mabaki ya miili hiyo kesho alfajiri kati ya saa 11 hadi 12,kisha ibada fupi kabla ya kuanza safari kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa maziko.
Sehemu ya mabaki ya nyumba ikiyoteketea kwa moto katika Kijiji cha Mjimwema,Usariver wilayani Arumeru ambapo kutokana na moto huo wamefariki watu watatu wa familia moja akiwemo bibi na wajukuu zake wawili. Picha na Janeth Mushi
“Tunategemea kesho kati ya saa 11 na 12 alfajiri kuchukua mabaki ya miili hiyo ambayo yamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti kilichopo Kituo cha Afya jirani na hapa,”
“Kisha tutakuja hapa nyumbani kutokanatutatoa heshima za mwisho na kuanzia saa mbili asubuhi tunatarajia kuanza safari kuelekea Msangeni kwa maziko kesho hiyo hiyo saa tisa alasiri baada ya shughuli za ibada kumalizika,”ameeleza
Tukio lilivyotokea
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo,Shedrack Antony,akisimulia namna tukio hilo lilivyotokea,amedai kuwa alfajiri ya siku hiyo walisikia kelele na walipotoka nje walishuhudia moto mkubwa ukiwaka katika nyumba ya bibi huyo aliyekuwa akiishi na wajukuu zake hao wawili.
Ameeleza kuwa walianza kuamshana ila walishindwa kuwaokoa waliteketea ndani kutokana na moto kuwa mkali na moshi kutanda sana.
“Huyu mama ni jirani yangu ilikuwa saa 11 alfajiri tulisikia kelele za kuomba msaada tulivyotoka nje tukaktuka moo umeshika nyumba upande mmoja,tukang’ang’ana kuvunja mlango kuwaokoa na tulivyovunja mlango tukamulika ndani moshi mkubwa ukawa umetanda,”
“Tukawa tunahangaika kutafuta walau kitambaa cha maji tujifunge ili kuingia kuwaokoa wlaiokuwa ndani,umeme ukaanza kupiga shoti na tukashindwa namna ya kuwaokoa,”ameeleza
Shahidi huyo amedai kuwa walizunguka upande wa pili kwenda kuvunja mlango wa nyuma lakini kufika kwenye mlango huo wa jikoni kuvuja mlango moto ulikuwa umeshaingia na gesi ikalipuka.
“Baada ya kusikia kishindo cha gesi tukakikimbia na tukawa tumeshapiga simu jeshi la zima moto na walifanya kwa haraka wakafika mapema na polisi walifika pia watu wakaambiwa wakae mbali, wakazima moto ila tukaingia tukakuta wametetekea wote.
Tulishindwa kuwaokoa,walipiga kelele kama mara mbili,”
Baadhi ya waombolezaji wakiwa ndani ya hema leo Alhamisi Aprili 30, 2026 katika msiba wa watu watatu wa familia moja ambao ni bibi na wajukuu zake wawili waliofariki baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto, katika Kijiji cha Mjimwema, Usariver Wilayani Arumeru. Picha na Janeth Mushi
“Mtoto huyo alikuwa napiga kelele anaita,mkubwa alishindwa kuhema na sehemu waliyokuwa moshi ulikuwa umetanda japo moto haukufika ila shoti ilikwamisha tusiweze kuwaokoa.Bibi kwa umri wake asingeweza kujiokoa,kuna muda alikuwa anapiga kelele anasema nisaidieni muwaokoe hata wajukuu wangu mimi nife tu,lakini moto ukawa mkubwa tukashindwa namna ya kuwaokoa,”amedai.
Shuhuda huyo ameeleza kuwa mtoto wa kiume (Jackson) alikuwa akipambana kuvunja mlango lakini kutokana na moshi kuwa mkubwa alishindwa kutoka na baada ya moto kuzimwa alikutwa amefariki mlangoni hapo.
“Mtoto mdogo alikuwa mlangoni anataka kumfuata bibi chumbani naye alifia hapo na bibi tumemkuta ameungulia kitandani, miili yao imeisha kabisa. Kiukweli ni tukio linalosikitisha sana.
Kwa upande wake,mtoto wa marehemu, Neema Msuya ameeleza kuwa kama familia wamepata pigo kubwa ambapo ameeleza binti yake alikuwa anasoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Amani na kuwa Jackson ni mtoto wa kaka yake.
“Kwa kweli tunasikitika tu na ukweli ni kwamba ni kwa mapenzi ya Mungu hakuna cha kuongea sana ila tunaomba watu tushirikiane kwa ajili ya kumaliza hili suala na mapenzi ya Mungu yatimizwe. Mtoto wangu Lerato alikuwa kipenzi cha bibi ndiyo maana sikumchukua nililmuacha aishi na bibi kwa sababu bibi anampenda sana akaendelea kukaa naye ningemchukua labda baada ya kumaliza darasa la saba na kumpeleka Sekondari,”
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Arusha, Oswald Mwanjegele akizungumzia tukio hilo amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.
“Kimsingi mpaka dakika hii, chanzo hakijabainika lakini ilikuwa ni jana, tulipokea taarifa kwamba eneo la Usa River, kuna tukio la moto kwenye nyumba ya Mkunde Kitio, alikuwa huko ndani na watu wengine wawili.
“Moto uliwaka, nyumba nzima ilishika moto. Kwa dalili zinavyoonyesha moto ulianzia sebuleni. Kwa hiyo moto ukawa umewazingira, wakawa wanapiga kelele kuomba msaada kwa majirani. Majirani wakaendelea kupambana na moto na ulipowazidi ikabidi wapige simu fire (zima moto),”amesema