
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka Saudi Arabia kusitisha hukumu ya kunyongwa kwa takriban Waethiopia 65 waliohukumiwa kifo kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Human Rights Watch inasema raia hao wa Ethiopia walihukumiwa katika vikao ambavyo viliwanyima haki zao za msingi.
Waethiopia watatu walinyongwa mnamo Aprili 21 kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya, ripoti hiyo ikisema walikuwa wamekimbia vita na umaskini, na kwamba walilazimishwa kubeba miraa au mirungi, mmea ambao ni halali nchini Ethiopia lakini marufuku nchini Saudi Arabia.
Nchi hiyo tayari imewanyonga watu 73 mwaka huu, ikiwa ni pamoja na watu 47 katika kesi za ulanguzi wa dawa za kulevya, kwa mujibu wa vyanzo vya habari.
Tangu Mwanamfalme Mohammed bin Salman achukue madaraka mnamo mwaka 2017 na licha ya kuahidi kukomesha hukumu ya kifo, zaidi ya watu 2,000 wameuawa wakiwemo watoto, wapinzani wa kisiasa na raia wa kigeni, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Mamia ya Waethiopia wanaaminika kuwa katika jela za Saudia Arabia.