
Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran (IRCS), katika kikao na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), ameitaka taasisi hiyo ya kimataifa kuiunga mkono Jumuiya ya Hilali Nyekundu na wananchi wa Iran katika kufuatilia kisheria ukiukwaji wa haki za kibinadamu katika vita vya siku 40 vya Marekani na Israel dhidi ya nchi hii.
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Bi Mirjana Spoljaric Egger, ambaye yuko ziarani nchini Iran kufuatilia athari vita hivyo, amefanya mazungumzo na rais wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran, Bw. Pir-Hossein Kolivand, siku ya Jumatano.
Akigusia tukio la kusikitisha la shambulio la adui dhidi ya shule ya Minab, Kolivand amesema kuwa katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya siku 40, nyumba za raia, watoto, wazee na watu wengine wasio na hatia walilengwa katika mashambulizi ya Marekani na Israel, na raia wengi waliuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya makombora na mabomu.
Akiwasilisha ripoti ya operesheni zilizotekelezwa na Hilali Nyekundu ya Iran wakati wa vita, alibainisha kuwa taasisi hiyo imefanya juhudi za mara kwa mara kurekodi matukio ya ukiukwaji wa sheria za kibinadamu, na tayari imeziwasilisha nyaraka husika kwa taasisi mbalimbali za kimataifa zinazoshughulika na masuala ya kibinadamu.
Kolivand aliendelea kufafanua kuwa vituo 56 vya Hilali Nyekundu vililengwa moja kwa moja na mashambulizi ya adui, helikopta tatu za uokozi ziliharibiwa, na magari 43 ya wagonjwa pamoja na magari mengine 49 ya uokozi yalilengwa moja kwa moja na Marekani na Israel katika kipindi cha vita.
Katika mkutano huo, Kolivand pia alirejea mauaji ya kikatili yaliyotokea katika siku ya kwanza ya vita katika mji wa Minab kusini mwa Iran, ambapo makombora ya Tomahawk ya Marekani yalilenga Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyibah, na kuua watu wasiopungua 175, wengi wao wakiwa wasichana wa shule.
Amesema juhudi za uokoaji katika mazingira ya maafa kama hayo, ambapo watoto walikuwa wahanga wakuu, zilikuwa miongoni mwa misheni za kuhuzunisha zaidi kwa wafanyakazi wa uokozi wa taasisi hiyo.
Kolivand amesema pia kuwa ufuatiliaji mpana tayari umefanywa kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).