Dar es Salaam. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ameomba Bunge kuidhinishiwa Sh222.5 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 ili kuwezesha utekelezaji wa vipaumbele vya wizara hiyo vinavyolenga kuimarisha uchumi wa kidijitali nchini.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni, Kairuki amesema wizara yake inatarajia kukusanya jumla ya Sh160.3 bilioni zitokanazo na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua inayoonesha mchango wa miundombinu hiyo katika kukuza mapato ya Serikali.

Kairuki amesema wizara imepanga kutumia kutumia Sh103.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao unatajwa kuwa uti wa mgongo wa huduma za kidijitali nchini.

Amezitaja kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuunganisha Mkongo wa Taifa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatua itakayoongeza wigo wa mawasiliano ya kikanda na kurahisisha biashara na uwekezaji.

Aidha, vituo 20 vitaunganishwa kwenye mkongo huo huku Serikali ikipanga kujenga vituo viwili vya kisasa vya kuhifadhi data (Data Centres) katika mikoa ya Dodoma na Zanzibar ili kuongeza usalama na uhifadhi wa taarifa za kidijitali.

Katika kuimarisha huduma za intaneti, amesema wizara itasimamia vituo saba vya mabadilishano ya intaneti (Internet Exchange Points) pamoja na kuwezesha huduma za Wi-Fi katika maeneo 100 ya umma nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mtandao kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wa sekta ya elimu amesema shule 100 zitaunganishwa na huduma ya mkongo kupitia maunganisho ya mwisho, jambo litakalosaidia wanafunzi na walimu kupata rasilimali za kujifunzia kwa njia ya mtandao.

Pia, Serikali imepanga kuimarisha miundombinu ya taarifa muhimu za kitaifa katika maeneo 100 ya umma pamoja na kuboresha Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam.

“Hatua nyingine ni kuunganisha taasisi 100 za haki jinai na ulinzi na usalama, zikiwemo mahakama, polisi, magereza na taasisi za kupambana na rushwa, ili kuboresha utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya kidijitali,” amesema Kairuki.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kati ya fedha zinazoombwa, Sh13.1 bilioni zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ikiwemo mishahara ya watumishi na gharama nyingine za uendeshaji, huku sehemu kubwa ya bajeti Sh209.4 bilioni sawa na asilimia 94.1 ikielekezwa katika miradi ya maendeleo.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, wizara imepanga kuwekeza Sh16.1 bilioni katika Mfumo wa Anwani za Makazi, unaolenga kurahisisha utambuzi wa maeneo na kuboresha utoaji wa huduma. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukamilisha sheria ya anwani za makazi, kuelimisha jamii na kuimarisha mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa taarifa hizo.

Pia, Sh13.7 bilioni zitatumika kujenga vituo vya kuendeleza ubunifu katika Tehama (ICT Parks), ambavyo vitasaidia kukuza ujuzi wa kidijitali kwa wananchi na kutoa mafunzo kuhusu teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili unde.

“Fedha hizo zinaombwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli kadhaa ikiwemo  kukuza ujuzi na maarifa ya kidijitali kwa wananchi, kufanya mafunzo kuhusu teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili unde,kuratibu utekelezaji wa miongozo mitatu ya Tehama na kuanzisha Mpango wa Kitaifa wa Mageuzi ya Kidijitali”amesema.

Katika kupeleka huduma vijijini, wizara imetenga Sh40 bilioni kwa mradi wa mawasiliano vijijini utakaohusisha ujenzi wa minara 636 pamoja na kubaini maeneo yenye changamoto za mawasiliano katika mikoa yote 31 nchini.

Aidha amesema kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Sh12.1 bilioni zitatumika kujenga Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali pamoja na vituo vya ubunifu katika kanda tano, sambamba na kuanzisha vituo 32 vya huduma pamoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali.

Katika hatua nyingine, Serikali imetenga Sh18.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali (NDTI), ambapo pamoja na ujenzi huo, wizara itatunga sheria ya kuanzishwa kwake na kuandaa mitaala ya mafunzo.

Kairuki amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo unalenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi unaoendeshwa na Tehama, huku ukitoa fursa zaidi za ajira, ubunifu na uwekezaji.

Mapendekezo ya kamati

Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mjumbe wa kamati hiyo, Abubakar Asenga amesema licha ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wizara na taasi zilizo chini ya wizara hiyo bado kuna mambo yanapaswa kufanyiwa kazi.

Amesema kamati hiyo inashauri Serikali ichukue hatua ya kuitambua Mamlaka ua Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama chombo cha kimkakati katika ulinzi na usalama wa Taifa na kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa na Mamlaka hiyo kama viashiria vya uvunjifu wa amani katika vyombo vya dola zinafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.

Kamati hiyo pia imeitaka Serikali kupanga na kutekeleza mkakati wa kuzuia na kupambana na uhalifu wa kimtandao ikiwa ni pamoja na wizi mitandaoni ikielekeza nguvu zaidi ielekezwe mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya na Rukwa ambapo matukio haya ni mengi.

Pendekezo hili limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Tume ya uchunguzi wa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi Oktoba 29, 2025 kueleza kuonesha mamlaka hiyo iliobaini mapema viashiria vya machafuko hayo.

Akiwasilisha taarifa ya tume hiyo Aprili 23,2026, mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Othman Chande alisema kuanzia Aprili hadi Oktoba 2025, TCRA ilikuwa ikiwasilisha taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama zikionesha kuwepo kwa viashiria vya ghasia vinavyolenga kuzuia na kuvuruga uchaguzi.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, Oktoba 17, 2025, TCRA iligundua kusambazwa kwa bango lenye maudhui ya kuchochea ghasia, likihamasisha maandamano yenye lengo la kuzuia na kuvunja uchaguzi mkuu.

Mbali na hilo, uchunguzi ulibaini mijadala mitandaoni iliyokuwa ikiendelea kuhusu mikakati ya kutekeleza ghasia siku ya uchaguzi.

“Majadiliano hayo yalionesha siku ya uchaguzi baadhi ya watu walipanga kuharibu mifumo ya umeme ili kuiingiza nchi gizani, kuchoma moto vituo vya mafuta pamoja na vituo vya kupigia kura kwa lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu.Viashiria hivyo vya mtandaoni vilikwenda sambamba na ushahidi wa mashahidi waliotoa taarifa mbele ya tume,” amesema.

Kamati hiyo pia imependekeza kufanyika kwa tathmini kuhusu matumizi ya vifurushi vya data na muda wa maongezi na kuja na utaratibu utakaomuwezesha mteja kutumia kifurushi chake mpaka kitakapoisha badala ya sasa ambapo anatumia hadi muda wa kifurushi utakapoisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *