
Pwani. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ametangaza hatua kali dhidi ya watumishi wa afya watakaoshindwa kutoa huduma kwa wajawazito kwa kisingizio cha kukosa fedha, siku chache baada ya gazeti la Mwananchi na The Citizen kuandika habari ya wajawazito kukumbana na changamoto ya huduma kutokana na fedha.
Mchengerwa amesisitiza kuwa uzembe huo hautavumiliwa na unaweza kugharimu ajira za watumishi hao, na yeyote atakayebainika Serikali itatwaa leseni yake na hataruhusiwa kuhudumu katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa 2026 iliyofanyika wilayani Kibiti, mkoani Pwani jana Jumatano, Aprili 29, 2026, Mchengerwa amesema licha ya Tanzania kupunguza vifo vya wajawazito kufikia 104 mwaka 2022, kutoka vifo 556 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2016, chanzo kingine ni uzembe unaosababishwa na watoa huduma za afya, akisema rushwa zinahusika na wengine kushindwa kutoa huduma, sababu kuu ikitajwa kukosa fedha za matibabu.
Mchengerwa amesema Serikali haitakubali kuona mjamzito akipoteza maisha au kupata madhara kwa sababu ya kucheleweshwa au kunyimwa huduma muhimu hospitalini.
“Sitakubali kusikia mjamzito analazwa sakafuni au anazuiwa kupata huduma kwa sababu hana fedha au amepoteza maisha kwa kushindwa kuhudumiwa kwa wakati. Hii siyo tu uzembe, bali ni ukiukwaji wa haki ya msingi ya Mtanzania kupata huduma bora za afya,” amesema Mchengerwa.
Amesema waganga wakuu wa mikoa na halmashauri watakaothibitika kushindwa kusimamia upatikanaji wa dawa katika vituo vyao watachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nafasi zao.
“Tumekubaliana na Mfamasia Mkuu wa Serikali (Daudi Msasi) na Mganga Mkuu wa Serikali (Grace Magembe) kuwa hakuna sababu ya Mtanzania kukosa dawa wakati takwimu zinaonesha upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 90. Huu upatikanaji haupaswi kubaki kwenye makaratasi, bali uonekane kwa mgonjwa anayefika kituoni,” amesema.
Waziri huyo amebainisha kuwa mgonjwa anayekosa dawa si tu anakosa tiba, bali anakosa haki yake ya kupata huduma bora, jambo ambalo Serikali haitalivumilia.
Katika kuelekea kuboresha huduma za afya nchini, Mchengerwa amesema Serikali imejikita katika kusogeza huduma karibu na wananchi ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Ametolea mfano ujenzi wa hospitali ya mkoa itakayohudumia wananchi wa Rufiji, Kibiti na Mkuranga, hatua itakayopunguza utegemezi wa hospitali za Temeke na Kibaha.
“Wananchi hawapaswi kusafiri kilomita 300 au 400 kutafuta huduma za msingi. Tunajenga hospitali hizi ili huduma zipatikane karibu yao, isipokuwa kwa matibabu ya kibingwa pekee,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imejenga vituo vya afya zaidi ya 3,500 na kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, hatua inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma stahiki kwa wakati.
Ripoti ya Mwananchi
Kuanzia Aprili 20 hadi 22, 2026, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kupitia magazeti na mitandao yake ya Mwananchi na The Citizen, ilipochapisha mfululizo wa habari kuonesha namna wajawazito wanavyohaha kusaka huduma za afya kutokana na kukosa fedha, kueleza umuhimu wa kundi hilo kupata huduma za afya bila kikwazo na mbinu za kufanikisha hatua hiyo.
Kupitia makala hizo ilinukuliwa Sera ya Afya ya mwaka 2007, sehemu ya 5.3.4 kifungu (c) (i), inayoelekeza matibabu bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanavyopaswa kupewa huduma, lakini haitekelezwi.
Sio sera hiyo tu, hata Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni, ambao Tanzania iliuridhia kuutekeleza mwaka 1976, wa kila nchi kulinda haki ya kila mtu kupata viwango vya huduma za afya vinavyozingatia utu na ubora, haukuzingatiwa.
Kulingana na wajawazito ambao Mwananchi ilizungumza nao katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro, walikiri kukosa huduma za afya kutokana na kukosa fedha Sh30,000 kwa ajili ya kuanza kliniki.
Pia, wanapokwenda kujifungua hutakiwa kubeba pamba, dawa za kuua vijidudu, glovu, sindano na plastiki za kujifungulia.
Kiwango hicho, walieleza, kinapaswa kutolewa punde tu mjamzito anapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza, na baadhi ya watoa huduma wa afya walieleza kuwa baadhi ya wajawazito wanatoka kwenye familia duni.
Kauli ya Mwigulu
Desemba 29, 2025, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi baada ya kukagua soko na stendi Bunju B, jijini Dar es Salaam, alisisitiza utekelezaji wa sera hiyo ya matibabu ya afya bure kwa wajawazito.
“Mjamzito akishafika hospitali asisubirishwe, sijui lete beseni, lete ndoo, afikishwe kwenye matibabu moja kwa moja. Kila hospitali iwe na mambo haya kwa ajili ya kusaidia Watanzania.
“Masuala ya uzazi siyo dharura, tunajua watoto wanakuja na nchi hii ni tajiri, haiwezi kukosa ndoo ya kumhudumia mama mmoja maskini,” alisema.