Arusha. Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha sekta ya fedha nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya amesema hayo leo Jumatano, Aprili 30, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuwa Serikali inalenga kufanya maboresho muhimu katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati.

‘’Rais Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa sekta binafsi na ameahidi kuendelea kufanya maboresho makubwa ya mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Dira 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka mitano ili kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, hasa sekta ya fedha na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi,” amesema Dk Chaya.

Amesema kufunguliwa kwa tawi hilo ni hatua muhimu ya kupanua huduma za PBZ Benki katika mikoa mbalimbali ya Tanzania hatua inayongeza ushindani, ujumuishaji wa kifedha na mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

‘’Napenda kutoa pongezi za dhati kwa PBZ Bank kwa hatua hii ya kimkakati ya kufungua tawi jipya katika Jiji la Arusha ambalo ni kitovu muhimu cha biashara, utalii, uwekezaji na huduma katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania,” amesema Dk Chaya.

Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, DkPius Chaya akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi wa tawi la PBZ Bank jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Naibu Waziri huyo, amesema sekta ya fedha ni moja ya sekta za kimageuzi za maendeleo ya uchumi wa kisasa na historia ya mageuzi ya sekta hiyo nchini imepitia hatua mbalimbali muhimu.

Amefafanua kuwa kabla ya mageuzi ya kiuchumi ya miaka ya 1990, sekta ya benki ilikuwa ikitawaliwa zaidi na taasisi za umma na huduma za kifedha zilikuwa na ushindani mdogo pamoja na upatikanaji hafifu wa mitaji kwa sekta binafsi.

‘’Kupitia mageuzi ya kiuchumi na kifedha, serikali ilifungua sekta ya benki kwa ushindani zaidi, ikawezesha kuanzishwa kwa benki binafsi, kuimarisha usimamizi wa Benki Kuu, pamoja na kukuza huduma za kisasa za kifedha zikiwemo benki za kidijitali, huduma za simu na mifumo ya malipo ya kisasa,” amesema.

Ameongeza kuwa sekta ya fedha hasa za mabenki imekuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya sekta binafsi kwa kuwezesha mitaji ya biashara, uwekezaji wa viwanda, biashara za kimataifa, pamoja na ukuaji wa biashara ndogo, za kati na kubwa.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya PBZ, Dk Juma Hassan Reli amesema ufunguzi wa tawi hilo siyo tukio la kawaida bali ni hatua muhimu ya kimkakati katika safari ya ukuaji wa PBZ Bank kusambaa zaidi hapa nchini.

“Arusha ni kitovu cha uchumi kinachokua kwa kasi, kikiwa na mchango mkubwa katika sekta za utalii, biashara, madini, kilimo pamoja na uwekezaji wa ndani na nje, hivyo uwepo wetu hapa ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kusogeza huduma bora za kifedha karibu zaidi na wananchi na wadau wa maendeleo,” amesema Dk Reli.

Amesema kupitia tawi hilo, PBZ Bank inalenga kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuwezesha ukuaji wa biashara ndogo za kati na kubwa na kutoa suluhisho bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja wa kisasa.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya (wa pili kulia) akiwa na Meneja wa PBZ Bank tawi la Arusha, Muna Nasser wakati wa uzinduzi wa tawi hilo, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Fahad Hamid na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi, Dk Juma Hassan Reli. Picha na Filbert Rweyemamu

Katika hafla hiyo pia imezinduliwa huduma yetu ya kidijitali ya “Lipa Hapa”, ambayo inalenga kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara na wateja kwa kutumia teknolojia ya kisasa, huduma hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendana na mapinduzi ya kidijitali na kuongeza ufanisi katika mifumo ya malipo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ Benki, Fahad Hamid amesema kwa sasa benki hiyo ni ya sita kwa ukubwa hapa nchini ikiwa na mali zenye thamani ya Sh3 trilioni ikiwa na kiwango kidogo cha mikopo chechefu ya asilimia mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *