MECHI ya Simba dhidi ya Yanga bado haijaisha, hiyo imefafanuliwa na mastaa wa zamani waliosema, kile walichokishuhudia kwenye fainali ya Kombe la Muungano 2026, kimetoa tafsiri wikiendi hii kazi itakuwa ngumu zaidi.

Mwanaspoti limezungumza na mastaa hao kwa nyakati tofauti na kutaja mambo matatu yanayoweza kuamua Kariakoo Dabi ijayo ambapo ni mbinu za makocha, mtazamo na Simba kuchoka kufungwa mara kwa mara na mtani wake Yanga.

Hatua hiyo imekuja baada ya juzi kushuhudia Simba ikiifunga Yanga bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Muungano, Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Ushindi huo umesitisha unyonge wa Simba mbele ya Yanga baada ya kupoteza mechi sita mfululizo za mashindano tofauti, kabla ya mara ya mwisho kutoka 0-0, kisha kupata ushindi juzi.

PUM 04

Jumapili hii, timu hizo zitakutana kwenye duru la pili la Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam na Simba itakuwa mwenyeji baada ya ile ya kwanza kumalizika kwa 0-0.

Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela amesema Wanamsimbazi waligundua udhaifu wao mapema hasa kwa upande wa kujizuia ambao ndiyo walifaulu, isipokuwa bado wanahitaji kujisahihisha kwenye umaliziaji.

“Mechi ilikuwa ngumu kwa pande zote mbili, Yanga pia ina shida katika kumalizia, hilo linatafsiri watakapokutana mechi ya ligi itakuwa ngumu zaidi, kwani kimbinu makocha wamefahamiana labda waje na plani nyingine, ninavyoona wanaweza wakagawana pointi,” amesema Mogela.

PUM 05

Jambo lingine alilolisisitiza Mogela kutokana na pafomansi ya mechi hiyo ni kuwafunza mashabiki kutokutembea na matokeo mfukoni.

Beki wa zamani wa Yanga na Stars, William Mtendamema, alielezea Pedro Goncalves mbinu zake zipo chini kidogo na ni zilezile katika mechi nyingi, lakini anaamini kama atasikiliza ushauri wa msaidizi wake, Abdihamid Moalin basi dabi ijayo kutakuwa na mabadiliko.

“Kocha wa Simba, Steve Barker mbinu zake ni za kimkakati na zimechangamka, kawachangamsha hadi wachezaji wake, mfano mechi hii Yanga ilipaswa kushinda kipindi cha kwanza au kipindi cha pili, kocha angekuja na mbinu mbadala, ila hilo halikuonekana,” amesema staa huyo na kuongeza;

PUM 06

“Mechi inayokuja itakuwa ngumu zaidi ya hiyo iliyopita, kwani Yanga haitataka kufungwa tena na ilianza mazoezi inaweza ikaifunga Simba muda wowote, Simba imechoka kufungwa na itataka kuionyesha Yanga wao ni watani wa jadi lazima kila mtu atacheka na kulia kwa zamu, kuhusu nani atashinda dakika 90 zitaamua.”

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi, amesema: “Simba imeanza kurejea katika makali yake ambayo yatafanya mechi ijayo iwe na presha kubwa, lakini iliyopita ya Muungano Cup timu zote zilikuwa na pafomansi kubwa, ingawa wachezaji wa Simba walikuwa na moyo wa kujitolea zaidi na mabeki wao walikuwa imara ndiyo kitu kipya kikubwa kilichoongezeka.”

PUM 01

Winga wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel, amesema: “Kiwango cha timu hizo, kimeziamsha timu zote mbili na mtihani wa kwenda kujipanga zaidi mechi ijayo, kabla ya fainali ya Muungano waliokuwa wanaonekana kujiamini zaidi ni Yanga, hivyo Simba kunyakua taji kumeamsha vita nyingine mpya, naamini wachezaji watarudi na viwango vya juu zaidi kwa mechi ijayo.”

Ameongeza: “Mechi ya mwisho ya ligi timu zilitoka suluhu na Simba ilionyesha kiwango kikubwa, awamu hii imechukua taji baada ya kukaa muda mrefu bila taji, hiyo ni tafsiri mapambano mapya, maana ni kawaida kuona Yanga ikiwa kwenye fomu basi Simba itayumba na Simba ikiwa kwenye fomu na Yanga inayumba katika harakati za kunyakua mataji.”

Katika mashindano ya Kombe la Muungano, Simba mechi tatu ilizocheza, imeondoka bila ya kuruhusu bao huku yenyewe ikifunga matano, ikishinda zote dhidi ya Mafunzo (1-0), Mlandege (3-0) na Yanga (1-0). Kwa upande wa Yanga, imeshinda mbili na kupoteza moja huku ikiruhusu mabao mawili wakati yenyewe ikifunga sita. Ilizifunga Muembe Makumbi City (4-0) na Azam (2-1), huku ikifungwa 1-0 na Simba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *