Arusha. Chama cha Wanasheria wa Afrika (Palu), kimesisitiza wajibu wa wanasheria barani humo ikiwemo kusimamia utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 30, 2026 na Ofisa Mtendaji wa Palu, Donald Deya akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) jijini Arusha.

Amesema kuwa kuna umuhimu wa kulinda maadili ya taaluma ya sheria na kusimamia haki za binadamu na kueleza kuwa vyama vya wanasheria vina jukumu kubwa kitaifa na kimataifa kuhakikisha misingi hiyo inalindwa na kuendelezwa.

“Na hii ni kitu kinachohitaji ujasiri kuna shida nyingi ambazo wananchi huwa wanazipitia hasa wakati wa uchaguzi,kwenye shida za kiuchumi. Kwa hiyo tunahitaji vyama vyetu vyote vya kitaifa,katika nchi 55 za bara letu wajitokeze,” amesema.

“Na tumehimiza sana TLS ijitokeze kusimamia utawala wa sheria na kulinda haki za kibinadamu na jamii,”amesema Ofisa huyo

Kwa upande wake Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi,amesema chama hicho kitaendelea kusimamia jukumu lake la kuhakikisha linasimamia haki kutendeka na sheria kusimamiwa ipasavyo.

“Hatufanyi biashara ya kuuza wajibu tunatekeleza wajibu,hapa ndipo penye kazi kubwa sana ambayo TLS tumekuwa tukipata changamoto hususani sisi viongozi.Kwa sababu baadhi wanashindwa kuelewa jukumu letu ni la kisheria,”amesema na kuongeza;

“Ninapotekeza jukumu langu usinitishe,ukikamata mtu ukamfikisha mahakamani mimi nikaja kumsaidia nikampa msaada wa kisheria, usimshambulie wakili wala kutisha TLS kwa sababu hatutakuogopa tutaendelea kutekeleza wajibu wetu,”

Ametaja moja ya changamoto ni matumizi yasiyo sahihi ya mamlaka hususani yanayofanywa na Jeshi la Polisi ambapo baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kukaa polisi kwa muda mrefu kinyume na sheria.

“Kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya mamlaka hususani yanayofwanuwa na Jeshi la Polisi kitendo hiki ni kile cha kukamata watu wanakaa nao muda mrefu kinyume na sheria, wakati kama kuna jambo unalichunguza sheria inakutaka uende mara moja kwa Hakimu aliyepo karibu utoe taarifa,” amesema.

“Wakati mwingine inawezekana nimuhimu kubaki na yule mtuhumiwa lakini fuata matakwa ya sheria watu wanakamatwa polisi ukienda wanakwambia hatuna huyu mtu baada ya wiki mbili wanasafirishwa kutoka point a hadi B,kinyume na utaratibu,” amesema.

Kuhusu changamoto ya maadili amesema iwapo wakili anakosea jambo kinyume na maadili hawatakubali hali hiyo.

“Kumekuwa na tabia sisi mawakili kujisahau kwenye nidhamu nilisema hili hatutalikubali ,tutaanza kulichukulia kwa umakini waliopewa maamuzi na hawataki kutekeleza hicho kikombe tutakunywesha kwa sababu hii ni taaluma lazima tuilinde,” amesema.

“Tunachukua kesi za wateja umepokea hela hutaki kuifanyia kazi ,unapewa maagizo na kamati yako ya maadili nenda katekeleze hufanyi,kuanzia mwezi Mei,2026 tutatekeleza ili tuhakikishe wananchi wako salama,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *