Morogoro. Huzuni na simanzi zimetanda katika Manispaa ya Morogoro kufuatia vifo vya watoto watatu waliodaiwa kuzama kwenye shimo la kokoto, huku mmoja wao akizikwa jana katika makaburi ya Kola na majirani wakilitaka Jeshi la Polisi kumkamata aliyelichimba shimo hilo.
Mtoto aliyezikwa ni Jackson Henry (2), mkazi wa mtaa wa Area Six, Kata ya Kichangani.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 28, 2026 majira ya jioni, ambapo watoto hao watatu Jackson Henry (2), Mikilia Rogath (4) na Mursin Ramadhani (4) walizama katika shimo lililokuwa limejaa maji ya mvua, likidaiwa kuchimbwa kwa ajili ya uchimbaji wa kokoto.
Mtoto Jackson Henry ( 2) enzi ya uhai wake.
Kwa mujibu wa majirani, miili ya watoto Mikilia na Mursin ilishazikwa katika maeneo tofauti, huku mmoja akisafirishwa kwenda Matombo na mwingine kuzikwa katika mtaa wa Mwande.
Akizungumza baada ya ibada ya mazishi, mjumbe wa Serikali ya mtaa, Salma Mlangwa, amesema licha ya onyo na hatua za awali kuchukuliwa dhidi ya mtu aliyelichimba shimo hilo, alikaidi agizo la kulifukia.
“Aliagizwa kulifukia na tuliamini ametekeleza, lakini baadaye tuligundua alikuwa akichimba kokoto usiku na kulifunika kwa miti asubuhi,” amesema.
Mama mzazi wa mtoto Jackson Henry mwenye umri wa miaka miwili aliyefariki baada ya kuzama kwenye shimo la kokoto (mwenye kilemba cheusi) akiingia kwenye gari kwenda kuzika mwili wa mtoto wake katika makaburi ya Kola Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
Amesema shimo hilo lilikuwa nyuma ya banda analoishi mtuhumiwa, eneo lisilo na njia wala muonekano rahisi, jambo lililochangia kuchelewa kugundulika kwa ajali hiyo.
Akisimulia mkasa huo, Mlangwa amesema watoto hao walikuwa wakicheza pamoja kabla ya kuelekea eneo hilo na kuanza kuchezea maji yaliyokuwa yamejaa shimoni. Baadaye wazazi walipoanza kuwatafuta bila mafanikio, waligundua miili yao ikielea majini ndani ya shimo hilo.
“Tangu walipotoka nyumbani hadi kupatikana kwa miili yao haikuzidi saa moja,” amesema.
Majirani wamesema wamepanga kushirikiana na Serikali ya mtaa kulifukia shimo hilo ili kuzuia madhara zaidi, huku wakisisitiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya mhusika.
Mjumbe mwingine wa mtaa, Hamisi Ramadhani, amesema tayari walishawahi kumfikisha mtuhumiwa katika vyombo vya utawala, lakini aliendelea na shughuli hizo kinyume cha maelekezo.
Shimo linalodaiwa kusababisha vifo vya watoto watatu ambao walizama kwenye shimo hilo lililokuwa likichimbwa kokoto mtaa wa area six kata ya Kichangani Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa huo, Habibu Degedela, amesema baada ya kukamilika kwa mazishi, suala hilo limekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.