Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya hususan maeneo ya pembezoni, juhudi mpya zimeelekezwa kwa vijana kupewa nafasi ya kuwa sehemu ya suluhisho ikiwa ni pamoja na ubunifu, ajira na uongozi ndani ya sekta hiyo.
Hatua hiyo inakuja sambamba na mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Taasisi ya Benjamin William Mkapa ambapo zaidi ya wataalamu wa afya 18,000 wamewezeshwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo yale ambayo ni magumu kufikika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano, Aprili 29, 2026 Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Ellen Senkoro amesema katika kipindi cha miaka 20, wameimarisha mifumo ya afya, hususani katika rasilimali watu na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Tunapoadhimisha miaka 20 ya Mkapa Foundation, tunaangazia urithi wa uongozi wenye maono, uwajibikaji na kujitolea kwa maendeleo ya watu, uliowekwa na hayati Benjamin William Mkapa,” amesema Dk Senkoro
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation, Dk Elllen Senkoro akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maadhimisho ya miaka 20 ya taasisi hiyo yatakayofanyika Julai, 2026 kulia kwake ni mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer.
Amesema mafanikio ya taasisi hiyo yamejengwa juu ya misingi imara tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 na kuendelezwa hata baada ya kifo cha mwanzilishi wake, huku uenyekiti wa bodi ukiendelea chini ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Kwa mujibu wa Dk Senkoro, katika kipindi hicho taasisi imefanikiwa kugusa maisha ya zaidi ya watu milioni 33 Tanzania Bara na Zanzibar kupitia miradi ya afya, hivyo wanafanya maadhimisho hayo kwa siku mbili kuanzia Julai 14 hadi 16 mwaka huu na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Naye, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer amesema mafanikio hayo yanaonekana zaidi katika namna taasisi hiyo ilivyoweza kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuajiri na kupeleka wataalamu wa afya katika maeneo yenye uhitaji mkubwa, hasa vijijini.
“Hawaajiri tu kwa ajili ya kujaza nafasi, bali wanaangalia maeneo yenye uhitaji mkubwa ambapo mara nyingi wataalamu wengi hawapendi kwenda, huko ndiko wanakopeleka nguvu kazi,” amesema Dk Laizer.
Amesema endapo kungekuwa na taasisi nyingi zaidi zenye uwezo na dhamira kama hiyo, Tanzania ingeweza kupiga hatua kubwa zaidi katika kuboresha huduma za afya.
Amesema wanataka kuelewa changamoto wanazokutana nazo vijana na namna sera zinavyoweza kuboreshwa ili kuwapa nafasi zaidi ya kushiriki kikamilifu.
Amesisitiza ushirikiano umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio hayo, akibainisha kuwa taasisi haiwezi kufikia malengo yake bila kufanya kazi bega kwa bega na serikali na wadau wengine.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Miradi na Mipango ya Kimkakati wa taasisi hiyo, Felician Luchagula, amesema washirika mbalimbali wa maendeleo, wawakilishi wa serikali pamoja na jukwaa la vijana watashiriki katika majadiliano yatakayolenga mustakabali wa sekta ya afya nchini.
“Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa la kutathmini mafanikio, changamoto na kuweka mikakati mipya ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi,”amesema Luchagula.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu wa Chama cha Startups Tanzania (TSA), Dk David Muhunzi amesema vijana wanapaswa kuwekwa mstari wa mbele katika kubadili mustakabali wa sekta ya afya barani Afrika.
Dk Muhunzi amesema licha ya Afrika kuwa na zaidi ya asilimia 60 ya watu wenye umri chini ya miaka 25, bado vijana hawajawakilishwa ipasavyo katika nafasi za maamuzi, hali inayowaathiri hata katika upatikanaji wa ajira.
“Kongamano hilo linalenga kujadili maeneo muhimu ikiwemo ubunifu wa kidijitali, uongozi wa vijana, mazingira ya kazi na ustahimilivu wa nguvukazi katika sekta ya afya,” amesema Dk Muhunzi.
Amesema kupitia mijadala, washiriki wanatarajia kuandaa azimio la vijana litakalowasilishwa kwa viongozi wa juu serikalini, likilenga kupendekeza hatua za kuboresha nafasi ya vijana katika mfumo wa afya nchini na barani Afrika kwa ujumla.