
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya ya jamii na wadau wa sekta ya viwanda wamesema suluhisho la kudumu katika udhibiti wa pombe haramu linapaswa kufanyika katika mnyororo mzima wa uzalishaji, hususan ethanoli ambayo ndiyo kiini kikuu cha utengenezaji wa pombe nyingi.
Wanashauri Serikali kuimarisha usimamizi wa uzalishaji, uingizaji na usambazaji wa kemikali hiyo ili kuziba mianya inayotumiwa na wazalishaji haramu sanjari na kutekeleza mkakati mpana wa udhibiti wa malighafi, matumizi ya teknolojia, elimu kwa umma na sera rafiki za kodi badala ya kutegemea misako na ukamataji pekee.
Hatua nyingine inayotajwa kuwa ya msingi ni matumizi ya teknolojia za kidijitali kufuatilia bidhaa kutoka kiwandani hadi kwa mlaji. Mifumo ya uthibitishaji inaweza kusaidia mamlaka kubaini bidhaa bandia sokoni, lakini pia kuwapa walaji uwezo wa kutofautisha bidhaa halali na feki kabla ya matumizi.
Kwa mujibu wao, mitandao mingi ya uzalishaji wa pombe haramu imejikita katika maeneo ya vijijini ambako mara nyingi hukubalika kijamii kama njia ya kujikimu. Ushirikiano na viongozi wa mitaa na vijiji unaweza kusaidia kuvunja mtandao huo kwa ufanisi zaidi kuliko operesheni za muda mfupi.
Kwa upande wa sera, wachumi wanashauri kuwepo kwa uwiano wa kodi kwenye pombe halali. Wanasema ongezeko kubwa la bei za bidhaa halali huwasukuma walaji wa kipato cha chini kutafuta mbadala wa bei nafuu, ambao mara nyingi huwa ni pombe haramu zisizo salama.
Mapendekezo hayo yanakuja wakati mjadala kuhusu athari za pombe haramu ukiendelea kushika kasi nchini, ukihusisha Serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
Mtafiti wa afya ya jamii, Dk Peter Mshana, alisema sheria zipo lakini utekelezaji wake haujawa sawa katika maeneo yote. “Katika baadhi ya maeneo ya vijijini, uzalishaji wa pombe haramu hufumbiwa macho au huonekana kama jambo la kawaida. Hapo ndipo tatizo linapoendelea kukua.”
Aliongeza kuwa mianya katika usimamizi wa ethanoli na ukosefu wa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji bado inawapa nafasi wazalishaji haramu kuendelea na biashara hiyo.
“Tunapongeza hatua ya Serikali kutoza kodi ethanoli kwenye chanzo. Hii ni njia muhimu ya kupunguza mianya ya biashara haramu,” alisema Dk Mshana.
Aidha, matumizi ya teknolojia yanapaswa kuongezwa zaidi. Mfumo wa kidijitali wa kufuatilia bidhaa unaweza kuwasaidia wasimamizi wa soko na pia kuwapa walaji uwezo wa kutambua bidhaa halisi.
Wataalamu pia wanashauri mamlaka kuhamia kwenye usimamizi unaoshirikisha jamii, kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo ya vijijini ili kuvunja mitandao ya uzalishaji haramu.
Elimu kwa mlaji imeelezwa kuwa nguzo nyingine muhimu. Watu wengi wanaonunua pombe hizo hawafahamu madhara makubwa ya kiafya wanayojikuta wakikabili.
“Mikakati endelevu ya elimu kupitia vyombo vya habari, shule na kampeni za kijamii inaweza kusaidia kupunguza mahitaji ya bidhaa hizi,” alisema Mchambuzi wa Uchumi Profesa Leonard Mbise.
Aidha, Mbise anaona kuna umuhimu wa kuwa na sera ya kodi yenye uwiano. Bei za pombe halali zinapopanda kupita kiasi, walaji wa kipato cha chini husukumwa kutafuta mbadala wa bei nafuu lakini usio salama.