
Siku chache baada ya mfanyabiashara maarufu barani Afrika, Aliko Dangote kuweka wazi dhamira ya kusaidia nchi za Afrika Mashariki kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta mkoani Tanga, wadau wa biashara na uchumi wamesema hatua hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi ya kiuchumi katika ukanda huu.
Mpango huo uliwekwa hadharani na Rais wa Kenya, William Ruto, aliyesema kuwa nchi za Afrika Mashariki ziko kwenye majadiliano ya pamoja ya kuanzisha kiwanda hicho katika Bandari ya Tanga, kikitarajiwa kujengwa kwa mfano wa kiwanda kikubwa cha Dangote kilichopo Nigeria.
Akizungumza katika mkutano wa ufadhili wa miundombinu uliofanyika jijini Nairobi wiki iliyopita, Ruto alisema kiwanda hicho kitakuwa cha kimkakati kwa ukanda mzima, kikitarajiwa kuchakata mafuta ghafi kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Sudan Kusini na Uganda.
“Nchi zetu zitanufaika kwa pamoja, kwa sababu kiwanda hicho kitahudumia soko la kikanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa za petroli kutoka nje,” alisema Ruto.
Kwa sasa, nchi nyingi za Afrika Mashariki zinaagiza karibu bidhaa zote za mafuta kutoka Mashariki ya Kati, hali inayozifanya kuwa katika hatari ya kukumbwa na misukosuko ya usambazaji na kupanda kwa bei pindi kunapotokea migogoro ya kisiasa katika eneo hilo, kama ilivyojitokeza hivi karibuni kufuatia mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati, ikiwamo Iran.
Katika mkutano huo, Dangote alisema yuko tayari kushirikiana na serikali za Afrika Mashariki kwa kutumia uzoefu na teknolojia ya kiwanda chake nchini Nigeria, ambacho kina uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku, iwapo kutakuwa na dhamira ya dhati ya kisera na uwekezaji kutoka kwa nchi husika.
Hatua hiyo inakuja wakati wananchi wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi wakiendelea kukabiliwa na ongezeko la bei za mafuta kutokana na changamoto za kimataifa, jambo lililoathiri kwa kiasi kikubwa sekta mbalimbali za uchumi ikiwamo usafirishaji, viwanda, kilimo na huduma.
Kwa mujibu wa wachambuzi, mzigo wa gharama hizo umeendelea kuhamishiwa kwa watumiaji wa mwisho kupitia kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, hali inayochochea mfumuko wa bei na kupunguza uwezo wa wananchi kumudu maisha.
Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Profesa Aurelia Kamuzora, anasema mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga ni hatua muhimu kwa maendeleo ya Tanzania na Afrika Mashariki, lakini utekelezaji wake unapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha unaleta manufaa yaliyokusudiwa.
Profesa Kamuzora anasema uzoefu wa mradi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) umeonyesha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inapopangwa vizuri inaweza kufanikiwa lakini ikiandaliwa vibaya inaweza kukwama au kushindwa kutekelezeka.
Ameeleza kuwa uwekezaji wa aina hiyo ni neema kwa taifa kwa sababu huleta mtaji, teknolojia mpya na mikataba kwa kampuni nyingi za ndani, huku vijana wenye ujuzi wakipata nafasi za ajira.
Anasema kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta kutarahisisha upatikanaji wa mafuta nchini, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuboresha mazingira ya uwekezaji.
“Migogoro ya kisiasa mara nyingi huathiri biashara, hivyo kuwa na uwezo wa ndani wa kusafisha mafuta ni hatua muhimu ya kujenga uchumi imara,” anasema.
Mchumi huyo anasema Afrika inapaswa kujitegemea kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zake badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje na kufanya hivyo litasimama imara zaidi kiuchumi kwani viwanda vya kutosha na bidhaa zinazozalishwa ndani.
Hata hivyo anaongeza kuwa ili kupata matokeo thabiti ni muhimu kuandaa soko la bidhaa hizo pamoja na walaji wake ili uwekezaji huo uwe na tija.
Naye Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude, anasema mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga ni mradi mzuri ambao ukifanikiwa utaleta mageuzi makubwa katika uchumi wa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.
Mkude anasema sekta ya viwanda ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi kwa sababu huongeza uzalishaji, hutengeneza ajira na kuingiza fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi lakini haiwezi kufanikiwa kama hakuna nishati ya kutosha.
Anasema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikiuza malighafi kwenda nje badala ya kuziongezea thamani hapa nchini, hali inayosababisha manufaa mengi kubaki mataifa mengine.
Anasema ndiyo sababu serikali imekuwa ikisisitiza sera ya local content katika miradi mikubwa ya kimkakati kama gesi asilia, madini ya kimkakati na mafuta, ili kuhakikisha wananchi na kampuni za ndani wanashiriki na kunufaika zaidi.
Kwa mujibu wake, nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kuondoa urasimu uliokithiri unaochelewesha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji.
Anasema wakati mwingine mazungumzo, vibali na taratibu nyingine huchukua muda mrefu kiasi cha kuwakatisha tamaa wawekezaji.
“Lazima kutakuwa na majadiliano kabla ya uwekezaji, lakini yakichukua muda mrefu sana mwekezaji anakata tamaa. Tukiepuka vikwazo hivyo tunaweza kufanikisha uwekezaji huu kwa haraka zaidi,” anasema.
Mkude anasema iwapo mradi huo utatekelezwa kwa wakati, utafungua fursa kwa sekta nyingine za mafuta na gesi kustawi, hasa kwa kuwa nchi nyingi za Afrika zinazozalisha mafuta kwa kiwango kidogo hulazimika kuyapeleka nje kusafishwa kwa gharama kubwa.
Ameeleza kuwa sekta ya uzalishaji ndiyo chanzo kikubwa cha ajira kwa wananchi wengi. Alisema kiwanda kimoja kinaweza kuajiri mamia ya watu moja kwa moja, na viwanda vingi zaidi vikijengwa idadi hiyo itaongezeka kwa kiasi kikubwa.
Aidha, anasema bidhaa zinazouzwa nje huingiza fedha za kigeni, wakati kuendelea kununua bidhaa zilizokwishazalishwa nje kunachangia kuzalisha ajira kwa mataifa mengine.
Mkude anasema mradi huo ni taarifa njema kwa Tanzania kwa sababu manufaa yake yatabaki nchini huku nchi jirani nazo zikinufaika kupitia biashara na huduma. Pia amesema uwepo wa kiwanda cha kusafisha mafuta ni moja ya njia za kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya kuendesha viwanda na mitambo mingine ya uzalishaji.
Hata hivyo, ameonya kuwa pamoja na kutungwa kwa sheria za kuvutia wawekezaji, wakati mwingine vitendo vinavyofanyika vinaweza kuwafukuza wawekezaji, hivyo ni muhimu sera na utekelezaji viende sambamba.