Tandahimba.  Siku moja baada ya Gazeti la Mwananchi kuripoti kuwepo kwa hofu miongoni mwa wazazi kufuatia uchakavu wa miundombinu katika Shule ya Msingi Namahonga unaohatarisha usalama wa wanafunzi, Serikali imeiagiza halmashauri husika kuchukua hatua za haraka kumaliza changamoto hiyo.

Mbali na shule hiyo iliyopo Kijiji cha Ujamaa, Kata ya Maundo, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, halmashauri hiyo pia imetakiwa kuzisaidia shule nyingine 17 zenye hali duni ili kuondoa kero zinazoikumba sekta ya elimu.

Shule ya Namahonga yenye zaidi ya wanafunzi 600 inakabiliwa na upungufu wa madarasa, ofisi, madawati na walimu; waliopo kwa sasa ni saba pekee, sita wakiwa wameajiriwa na mmoja wa kujitolea, hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

Jana mjadala uliibuka katika Kikao cha Baraza la Madiwani kuhusu hali ya shule hiyo, huku Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmad akiitaka halmashauri kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto hizo.

Jengo la ofisi ya walimu wa shule ya msingi Namahonga

Akizungumza kwenye kikao hicho jana Jumatano Aprili 29, 2026, Katani ameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kuweka mkazo katika kuboresha mazingira ya elimu, akieleza kuwa hali ya Shule ya Namahonga, si rafiki kwa ujifunzaji.

“Watu wamefika Namahonga na kupiga picha za madarasa yale, lakini wameishia hapo tu. Wangefika katika shule nyingine za msingi katika jimbo hili, wangekuta kuna takribani shule 17 zenye hali kama hiyo,” amesema.

“Gazeti la Mwananchi limechapisha picha ya Shule ya Msingi Namahonga, nawashauri mfungue simu zenu mjionee. Hata mimi napokea simu na ujumbe mwingi watu wakiniuliza, ‘Hiyo Tandahimba ndiyo Doha uliyoisema?’” amesema mbunge Katani.

Amesisitiza umuhimu wa halmashauri kuweka kipaumbele katika kutatua kero za msingi zinazogusa wananchi moja kwa moja, ikiwamo elimu, afya na maji.

Majengo ya madarasa la shule ya msingi Namahonga

“Ni kweli kuna changamoto ya uhaba wa vitendea kazi kwa watumishi wetu, lakini kwa muda tunaweza kuazimana badala ya kutumia fedha nyingi kununua magari na fedha hizo zikaelekezwa hata Namahonga,” amesema.

Katani pia amewataka wataalamu wa halmashauri kupitia upya vipaumbele vya matumizi ya fedha ili rasilimali zielekezwe katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kwa wananchi na jamii kwa jumla.

“Mimi sina pingamizi na ununuzi wa gari, lakini kwa hali ilivyo katika shule zetu, zinahitaji maboresho ya haraka. Nimetembelea mwenyewe na kuona hali halisi; tunajivunia makusanyo ya Sh7 bilioni, lakini wanafunzi wanateseka, sasa kipaumbele ni gari au wananchi?” amehoji.

Akichangia hoja hiyo, diwani wa Mahuta, Mamlo Muhammad amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya kiutendaji ya halmashauri iwapo kifungu hicho hakiwezi kubadilishwa.

“Kama fedha hii haiwezi kufanyiwa marekebisho, basi ni bora itumike kununua gari kuliko kugawanywa kwenye posho, au kama kuna uwezekano wa kubadili matumizi basi hilo lifanyike,” amesema Mohamed.

Majengo ya madarasa ya shule ya msingi Namahonga.

Diwani Marijani Linguvi amesema, “Wenye mamlaka ya mwisho ya matumizi ya fedha hizi ni sisi madiwani, hivyo tutumie busara kwa kugawa fedha hii; sehemu iende kwenye elimu na nyingine itatue changamoto nyingine za wananchi.”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Mariam Mwanzalima amesema matumizi ya fedha za umma yanaongozwa na taratibu na miongozo ya bajeti, hivyo hayawezi kubadilishwa kiholela.

“Matumizi ya fedha za umma yana utaratibu wake; miradi hutekelezwa kwa kuzingatia sera za maendeleo na vifungu vyake, hivyo utekelezaji wa bajeti hufuata mwongozo uliopo,” amesema.

“Suala la Shule ya Namahonga tayari limeshafanyiwa kazi; wataalamu walitembelea shule hiyo na kubaini kuwa madarasa yaliyopo hayawezi kukarabatiwa, hivyo zimetengwa Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya,” amesema Mariam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *