Dodoma. Katibu wa Bunge la Tanzania, Baraka Leonard ametangaza uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za wabunge watatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) huku majina matatu yakiwa tayari yametangazwa.

Uchaguzi huo utafanyika Jumatatu ya Mei 4, 2026 ambapo walioteuliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni Cosato Chumi, Kambarage Wasira na Fatuma Abdallah Kange ambao watapigiwa kura kwa mujibu kanuni za uchaguzi kwa nafasi hiyo.

Wabunge hao wanachaguliwa kuziba nafasi za wabunge watatu ambao kwa mujibu wa kanuni za Bunge la Afrika Mashariki uwakilishi wao umekoma baada ya kuchaguliwa na kuteuliwa kuwa wabunge wa Bunge la Tanzania.

Wabunge hao walikuwa ni James Ole Milya ambaye katika uchaguzi mkuu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Simanjiro, Dk Ngwaru Maghembe (Mwanga) na Angela Kizigha ambaye Aprili 2, 2026 aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mbunge.

“Uchaguzi huu mdogo unafanyika kwa mujibu wa kanuni ya 20 ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2025 ambayo inaeleza uchaguzi mdogo unapaswa kufanyika ili kujaza nafasi iliyowazi,” amesema Leonard.

Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 51(3) ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ya 1999 ikisomwa pamoja na kifungu cha 7(3) cha sheria ya uchaguzi ya Bunge la Afrika Mashariki namba 4 ya mwaka 2011 kwamba waliochaguliwa kuwa wabunge katika Mataifa yao hawawezi kuendelea kutumikia Bunge la Afrika Mashariki.

Tangazo la uchaguzi wa wabunge hao lilitolewa April 14, 2026 katika Gazeti la Serikali na katika vyombo vya habari ili kuutaarifu umma kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo ambapo leo Aprili 30, 2026 ilipangwa kuwa siku ya uteuzi.

Leonard amesema hadi saa 10:00 jioni ya leo Alhamisi, Aprili 30, 2026, ofisi yake ilipokea fomu na stakabadhi za malipo ya ada ya kugombea kutoka kwa wagombea watatu ambao ni Fatuma Abdallah Kange, Kambarage Wasira na Cosato Chumi ambaye amewahi kuwa mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Mkoa wa Iringa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Amesema itakapowadia siku ya uchaguzi,kabla ya wabunge kupiga kura, wagombea wataruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge, watajitambulisha na wataomba kura kwa lugha ya Kiingereza.

“Baada ya hatua hiyo, wabunge watapewa fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa idadi itakayoamuliwa na Spika. Kisha zoezi la kupiga kura litaanza, kura zitahesabiwa na washindi watatangazwa,” amesema.

Watatu hao wamepatikana baada ya mchakato wa ndani wa CCM wa kuchukua na kurejesha fomu na jana Jumatano, Aprili 29, 2026, Kamati Kuu ya chama hicho, chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan iliwateua wana CCM tisa, kati yao sita wanaume.

Baada ya uteuzi huo ulioshuhudia majina ya waliokuwa wabunge na wale walioshiriki kura za maoni ndani ya chama hicho za kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 wakijitosa kuwania ubunge wa EALA.

Miongoni mwao wamo waliowahi kushika nyadhifa za juu Serikalini, wakiwemo waliowahi kuwa manaibu mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa nyakati tofauti.

Wanasiasa hao ni Stephen Byabato na Cosato Chumi, waliokuwa wabunge wa majimbo ya Bukoba Mjini na Mafinga Mjini (Iringa). 

Wawili hao walishindwa kupenya katika hatua tofauti za uteuzi na kura za maoni za ndani ya CCM, hatua iliyowafanywa kushindwa kupata nafasi ya kutetea majimbo yao.

Siyo hao tu, yumo Kambarage Wassira aliyewania ubunge wa Bunda Mjini, lakini hakufanikiwa kupenya badala yake kamati kuu ya CCM kurudisha jina Ester Bulaya.

Mbali na hao, kikao hicho kiliwapitisha Chikulupi Kasaka, Fatuma Kange na Jesca Mshama, kwa upande wa wanawake kuwania nafasi ubunge wa EALA

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, wengine walioteuliwa ni Jabir Bwanika na Dk Suleiman Serera na Paschal Masalu.

Pia, ilisema watapigiwa kura na wabunge wa CCM ili kupata majina mawili ya wanaume kati ya sita na mmoja kati ya watatu kwa wanawake ili kujaza nafasi hizo tatu zilizo wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *