Dar es Salaam. Serikali imebaini na kufungia jumla ya laini za simu 62,879, pamoja na kuzuia kufanya usajili wa laini mpya za simu kwa Vitambulisho vya Taifa (Nida) 60,177 vilivyohusika katika matukio ya ulaghai.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Aprili 30, 2026, bungeni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huu akiomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh222 bilioni.

Kwa mujibu wa Kairuki, katika ya Machi 2025 hadi Machi 2026, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebaini na kufungia jumla ya laini za simu 62,879, pamoja na kuzuia kufanya usajili wa laini mpya za simu kwa vitambulisho vya Nida 60,177 vilivyohusika katika matukio ya ulaghai.

Hatua hizo za wizara ni muendelezo wa hatua zilizoanza kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye, aliyeanzisha vita dhidi ya matapeli wa mtandaoni wanaotumia mbinu kadhaa, ikiwamo ya “tuma kwenye namba hii”, aliyesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo hivyo.

Pia, aliwahi kutangaza kuzima laini zilizokuwa hazijahakikiwa, ikiwamo kuwataka wenye Nida kufanya uhakiki kuona kama hakijatumika kusajili laini nyingine zisizofahamika.

Akihutubia bungeni leo, Waziri Kairuki amesema kupitia TCRA, Serikali imeendelea kudhibiti huduma za mawasiliano ya simu nchini.

“Kukua kwa teknolojia kunapelekea baadhi ya wananchi wasiokuwa na nia njema na nchi yetu kufanya matukio ya utapeli.

“Ili kudhibiti matukio hayo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea kuboresha na kusimamia uendeshaji wa mfumo wa ufuatiliaji wa mawasiliano, unaosimamia na kudhibiti huduma za mawasiliano ya simu nchini.

“Mfumo huu umeiwezesha mamlaka kubaini simu za ulaghai, ikiwemo utapeli kwa njia ya mitandao. Katika kipindi cha Machi 2025 hadi Machi 2026, mamlaka imebaini na kufungia jumla ya laini za simu 62,879, pamoja na kuzuia kufanya usajili wa laini mpya za simu kwa vitambulisho vya Taifa 60,177 vilivyohusika katika matukio ya ulaghai,” amesema.

Kuhusu matapeli wa “tuma kwenye namba hii”, Nape aliwahi kutoa ushuhuda bungeni kwamba aliwahi kulengwa na matapeli hao, alisisitiza kuwa utapeli huo umekithiri na kuwataka vijana kuacha tabia hiyo ya uhalifu.

Alitaja jitihada zilizofanywa na Serikali kupitia TCRA, ikiwamo kufuta laini zote zinazobainika kutumika kwenye utapeli, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku Nida zilizosajili namba hizo.

Pia, Jeshi la Polisi liliendelea kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahusika wanaopatikana na hatia ya utapeli wa “tuma kwa namba hii”.

TCRA ilizindua kampeni ya ‘Sitapeliki’ kwa kutoa elimu kwa umma kuripoti matapeli ili kupunguza wimbi la utapeli, ikitaja hatua za kuchukua, ikiwamo kutuma namba ya simu iliyokupigia au ujumbe wa utapeli kwenda namba 15040 bila malipo ili ifungiwe.

Pia, kutuma neno “Utapeli” kwenda 15040, ukifuatiwa na namba ya simu ya tapeli, na kupiga *106# kuona namba zote zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako cha Nida na kuripoti namba usizozijua.

Huduma za TTCL

Kuhusu Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL_, Waziri Kairuki amesema wizara kupitia shirika hilo imefanikiwa kufikisha huduma ya Wi-Fi katika maeneo ya umma 50, hivyo kufanya jumla ya maeneo yaliyounganishwa kufikia 61 kati ya 120, sawa na asilimia 51 ya lengo lililokusudiwa.

Amesema maeneo yaliyofikishiwa huduma ni pamoja na masoko, stendi kuu za mabasi, hospitali za rufaa za mikoa, vyuo vikuu na vya kati, pamoja na maeneo ya umma.

Waziri Kairuki amesema maeneo hayo yapo katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Geita, Pwani, Pemba, Unguja, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC)

Akizungumzia kuhusu Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Waziri Kairuki amesema imepokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko kuhusu madai ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu 155.

“Mheshimiwa Spika, tume imepokea ripoti ya uvunjifu wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi kutoka kwa taasisi saba na imepokea na kushughulikia malalamiko 55 ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi.

“Aidha, tume imetoa ushauri katika ripoti za uzingatiaji kwa taasisi 900, ushauri wa sera za ulinzi wa taarifa binafsi kwa taasisi 22 na imetoa vibali 38 vya kusafirisha taarifa nje ya nchi,” amesema.

Pia, amesema wizara imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ulinzi na usalama wa mtandao kwa makundi mbalimbali ya jamii, ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma, wanafunzi, wajasiriamali wa kidijitali, vikundi vya kijamii kama waendesha magari na bodaboda, Vicoba na wananchi.

“Elimu hii imekuwa ikitolewa kwa njia mbalimbali, ikiwamo redio, televisheni, mitandao ya kijamii, pamoja na kutembelea shule za msingi na sekondari, na wananchi takribani milioni nne walifikiwa,” amesema.

Polisi kufuatilia makosa ya mtandaoni

Waziri Kairuki amesema wizara imewezesha uandaaji wa mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji wa matukio na makosa ya mtandao nchini, unaosimamiwa na kutumika na Jeshi la Polisi.

Amesema mfumo huo utawezesha kuimarisha ulinzi na usalama mtandaoni kwa kuhakikisha mazingira salama ya matumizi ya Tehama.

Waziri Kairuki amesema wizara imeanzisha jumuiya za usalama mtandao katika vyuo mbalimbali nchini.

Amesema jumuiya hizo zinalenga kuwatambua vijana wenye uelewa na hamasa katika masuala ya usalama wa mtandao na kuwajenga kimaadili ili kuhimiza matumizi sahihi na salama ya mtandao.

“Hadi Machi 2026, wizara imefanikiwa kuanzisha jumuiya hizo katika vyuo sita vya UDOM (Chuo Kikuu cha Dodoma), UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), IAA (Chuo cha Uhasibu Arusha), ATC (Chuo cha Ufundi Arusha), DIT (Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam) na IFM (Chuo cha Usimamizi wa Fedha).”

Amesema pia wizara imeanzisha jukwaa la mawasiliano linalowaunganisha viongozi wa jumuiya za usalama wa mtandao katika vyuo husika ili kuendelea kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya mtandao.

Kamati ya Miundombinu

Akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abubakar Asenga, ambaye pia ni mbunge wa Kilombero, ametaja maoni kadhaa ya kamati hiyo.

Kwa mujibu wa kamati, Serikali ichukue hatua ya kuitambua TCRA kama chombo cha kimkakati katika ulinzi na usalama wa taifa, na kuhakikisha kuwa taarifa zinazowasilishwa na mamlaka hii kama viashiria vya uvunjifu wa amani katika vyombo vya dola zinafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.

“Ipange na kutekeleza mkakati wa kuzuia na kupambana na uhalifu wa kimtandao, ikiwa ni pamoja na wizi mitandaoni.

“Aidha, nguvu zaidi ielekezwe katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya na Rukwa, ambako matukio haya ni mengi,” amesema Asenga.

Pia, kamati imetaka wizara ifanye tathmini kuhusu matumizi ya vifurushi vya data na muda wa maongezi na kuja na utaratibu utakaomwezesha mteja kutumia kifurushi chake mpaka kitakapoisha, badala ya sasa ambapo anatumia hadi muda wa kifurushi utakapoisha.

Kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi, kamati imeshauri kuwa Serikali iandae mkakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya mitandao na madhara ya kuweka taarifa binafsi katika mitandao ya kijamii ili kuhakikisha jamii inazingatia faragha na kupunguza uhalifu na unyanyasaji wa kimtandao nchini.

Pia, kamati imeshauri Serikali itoe elimu na mwongozo mahususi kwa watumishi wa umma na sekta binafsi kuhusu umuhimu wa kutunza taarifa binafsi za wateja pamoja na taasisi wanazozifanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria watumishi watakaobainika kushindwa kutekeleza masharti ya mwongozo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *