Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha siku 10 kuanzia Mei Mosi hadi Mei 10, ikieleza kuwa mvua zitaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini, hasa kanda ya Ziwa Victoria, ukanda wa Pwani na baadhi ya nyanda za juu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika maeneo kadhaa ndani ya kipindi hicho.

Katika nyanda za juu kaskazini-mashariki, zinazojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo machache, huku ukanda wa pwani ukiendelea kushuhudia hali ya unyevunyevu.

“Mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya TMA.

Kwa upande wa magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora itapata vipindi vya mvua vinavyoambatana na radi, ingawa katika maeneo machache.

Hata hivyo, hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea katika kanda ya kati, hususan mikoa ya Dodoma na Singida.

Katika nyanda za juu kusini-magharibi, zinazojumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, vipindi vya mvua vinatarajiwa kutokea kwa uchache.

Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika ukanda wa kusini, ukiwemo mkoa wa Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro.

Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara katika ukanda wa Pwani ya kusini, mvua zinazoambatana na radi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo.

TMA imeeleza kuwa hali hiyo ya mvua inachangiwa na mabadiliko ya mifumo ya migandamizo ya hewa duniani.

Kulingana na taarifa hiyo, katika kipindi cha siku 10, migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena na Mascarene) inatarajiwa kuendelea kuimarika wakati ile iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) ikitarajiwa kuendelea kudhohofika

 “Hali hii inasababisha ukanda wa mvua kusogea kuelekea kaskazini, na hivyo kuimarisha mifumo ya mvua katika maeneo ya Ziwa Victoria, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Pwani,” imefafanua TMA.

Aidha, kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa katika ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na upepo wenye unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi kunatarajiwa kuongeza uwezekano wa mvua katika maeneo ya Pwani na maeneo ya jirani.

Kwa ujumla, mamlaka hiyo imewataka wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua zenye radi, huku wakifuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zitakazokuwa zikitolewa mara kwa mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *