Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka waajiri na wafanyakazi nchini kujiandaa kukabiliana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoendelea duniani, akisema hali hiyo inaathiri moja kwa moja maisha ya Watanzania na mataifa mengine yanayoendelea.

Akihutubia maelfu ya wafanyakazi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe leo Mei 1, 2026, Rais Samia amesema dunia inapitia kipindi kigumu kiuchumi kinachosababishwa na sababu mbalimbali, hali inayoongeza gharama za maisha kwa wananchi.

Amesema licha ya changamoto hizo, Serikali imejipanga kuhakikisha maisha ya Watanzania hayaendi nyuma, bali yanabaki katika kiwango kilichopo au kuboreka zaidi kadri hali itakavyoruhusu.

“Ugumu unaanza serikalini kwanza, ndipo unaenda kwa wengine. Tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wetu hawashuki kutoka hapa walipo,” amesema Rais Samia.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia amelipongeza Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kwa kuonesha uzalendo kwa kutowasilisha madai mapya ya nyongeza ya mishahara mwaka huu, akieleza kuwa uamuzi huo unaonesha uelewa wa hali halisi ya uchumi.

Wafanyakazi wa wizara mbalimbali, taasisi za umma na binafsi wakipita mbele ya jukwaa kuu katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi 2026) ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Njombe leo Ijumaa Mei Mosi 2026.

Amesema viongozi wa Tucta walichagua kuipa pole Serikali badala ya kuibana kwa madai, hatua aliyosema inaashiria mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki kigumu.

“Tucta wamesema mwaka huu tufunge mkanda, mwakani watakuja kudai. Nami nimesema tukichapa kazi na uchumi ukakua, tutakaa tuangalie namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi,” amesema.

Akizungumzia sababu za hali ya sasa ya uchumi, Rais Samia amesema Serikali ilitumia fedha nyingi kugharamia uchaguzi uliopita kwa asilimia 100, hali iliyosababisha kubana matumizi katika maeneo mengine.

Maofisa wa Polisi wakipita mbele ya jukwaa kuu katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi 2026) ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Njombe leo Ijumaa Mei Mosi 2026.

Aidha, ametaja uharibifu wa mali na miundombinu uliotokea wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025 pamoja na athari za mvua kubwa zilizoharibu barabara na miundombinu mingine kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia shinikizo la kiuchumi.

Kutokana na hali hiyo, amesema mapato yanayokusanywa kwa sasa yanaelekezwa zaidi katika ukarabati wa miundombinu na ulipaji wa madeni ya ndani, yakiwemo ya wafanyakazi na wakandarasi.

“Tumeamua kulipa kwanza madeni sugu ili tunapoanza utekelezaji wa dira mpya ya maendeleo, tuanze tukiwa na msingi mzuri,” amesisitiza.

Akizungumzia mustakabali wa ajira, Rais Samia amesema mabadiliko ya teknolojia yanabadilisha kwa kasi namna kazi zinavyofanyika, hivyo kuhitaji nguvu kazi yenye ujuzi mpya na maarifa ya kisasa.

Ametoa wito kwa sekta binafsi na umma kuwekeza katika elimu na mafunzo ya ujuzi ili kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

“Ajira za kesho zitahitaji ujuzi wa juu zaidi, matumizi ya teknolojia na ubunifu. Hatuwezi kuendelea na mfumo wa zamani wa uzalishaji,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kurasimisha sekta isiyo rasmi ambayo imeajiri idadi kubwa ya Watanzania, ili kuongeza mchango wake katika uchumi na kuwapatia wafanyakazi hao ulinzi na fursa zaidi.

Kuhusu masilahi ya wafanyakazi, Rais Samia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuyaboresha kadri uchumi utakavyokua, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi.

Wafanyakazi wa wizara mbalimbali, taasisi za umma na binafsi wakipita mbele ya jukwaa kuu katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi 2026) ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Njombe leo Ijumaa Mei Mosi 2026.

Akigusia kauli mbiu ya mwaka huu, Rais amesema hakuna kazi yenye staha bila kuwepo kwa amani na utulivu, hivyo amewataka wananchi kulinda misingi hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Amesisitiza kuwa tofauti za maoni zisigeuke chanzo cha kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa, akionya kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Tusilinde tu haki zetu za kazi, bali tulinde pia amani ya nchi yetu. Bila amani, hakuna maendeleo wala ustawi wa wafanyakazi,” amesema.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Rais wa Tucta Tumaini ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 35 kwa madaraja yote mwaka uliopita.

Amebainisha kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kipekee kwani hakuna mtumishi aliyekosa nyongeza hiyo.

 Ameongeza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika upandaji wa madaraja, jambo ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya watumishi.

Mbali na masilahi ya watumishi wa umma, Tucta imempongeza Rais kwa kufungua milango ya ajira, hususan fursa za kazi nje ya nchi.

 Ameeleza kuwa Novemba mwaka jana hadi sasa, vijana zaidi ya 6,000 wameshasafiri kwenda kufanya kazi nje ya nchi, hatua inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.

Kuhusu sekta binafsi, kiongozi huyo wa Tucta ameeleza kuwa utekelezaji wa kima cha chini cha mshahara uliopitishwa na kuanza kulipwa Januari mwaka huu umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Wafanyakazi wa wizara mbalimbali, taasisi za umma na binafsi wakipita mbele ya jukwaa kuu katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi 2026) ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Njombe leo Ijumaa Mei Mosi 2026.

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya waajiri tayari wameanza kutekeleza viwango hivyo, huku wakishirikiana na wizara husika kuwafuatilia waajiri wachache wanaolete usumbufu ili wachukuliwe hatua.

Pamoja na mafanikio hayo, Tucta imeiomba Serikali kuitazama kwa jicho la kipekee changamoto ya miundo ya utumishi.

Nyamhokya ameeleza kuwa watumishi wengi wanapata wakati mgumu wanaporudi kutoka masomoni baada ya kupata shahada lakini wanalazimika kuendelea na mshahara wa zamani au kuanza upya kama walioajiriwa siku hiyo.

Akitoa salamu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), Mwakilishi wa shirika hilo Afrika Mashariki, Caroline Mugala, amesema maendeleo yanayoshuhudiwa sasa nchini, yanaakisi nguvu ya ushirikiano wa utatu katika sekta ya kazi na ajira.

Ameeleza kumeshuhudiwa mafanikio kadhaa katika sekta ya kazi, ikiwemo uzinduzi wa mpango wa taifa wa kazi zenye staha.

Amesema mpango huo unathibitisha dhamira ya Taifa ya kuweka kipaumbele katika kazi zenye staha katikati ya mipango ya maendeleo, utekelezaji na ufikiaji wa malengo ya Dira ya 2050.

Caroline, amesema zaidi ya vikundi 14,000, kati yao asilimia 66 wanawake wameshiriki katika ukarabati na utunzaji wa zaidi ya kilomita 1,500 za barabara za vijiji na kujiingizia kipato cha zaidi ya Sh2 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *