Mtama. Wafanyakazi 300 wanatarajiwa kuajiriwa katika kiwanda cha kubangua korosho kinachojengwa katika eneo la Kiwalala Halmshauri ya Mtama mkoani Lindi.
Ujenzi wa kiwanda hicho cha kubangua korosho kinatarajiwa kukamilika ifikapo 2028 na ujenzi wake utagharimu kiasi cha Sh1.2 bilioni na utweza kuajiri wafanyakazi 300.
Mradi wa ujenzi wa kiwanda cha ubanguaji wa korosho unaotekelezwa na Watanzania wazawa kupitia Kampuni ya Quickstep Investment Limited itakuja kuondoa changamoto ya soko la wakulima wa korosho katika mikoa ya kusini.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 1,2026 Meneja wa kiwanda hicho Said Mrisho,amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kubangua korosho Tani elfu 50 kwa mwaka ambnapo kwa mwezi kitabangua Tani 4000.
Amesema kuwa shughuli zitakazofanyika katika kiwanda hicho ni pamoja na kuhifadhi korosho, upimaji wa mizigo kwa kutumia mizani pamoja na ubanguaji wa korosho.
“Awamu ya kwanza tayari tumetoa ajira tano za kudumu na ajira 40 za muda, huku mradi mzima ukitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 300 mara utakapokamilika.”amesema Mrisho.
Mrisho amesema kuwa mradi huo pia unatarajiwa kufungua fursa nyingi zisizo rasmi kupitia mnyororo wa thamani kwa wafanyabishara wadogowadogo kama mama lishe, Baba lishe.
Kiwanda cha kubangua korosho kinachojengwa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama katika kijiji cha Kiwalala ambacho kitaajiri wafanyakazi 300.Picha na Bahati Mwatesa
Pia amesema kiwanda hicho kitasaidia kutoa soko la uhakika kwa wakulima wa korosho kupitia vyama vya ushirika na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa nchini pamoja na Halmashauri ya Mtama kwa kuwapatia ardhi na huduma za upimaji.”amesema Pia
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amesema kuwa uwekezaji unayofanyika utaleta mapinduzi ya uchumi kwani wakulima wa korosho watakuwa wanauza kwenye kiwanda hicho,pia amesisitiza wakulima pindi mradi utakapokamilika wakulima wajitahidi kupeleka korosho zenye ubora ili kupata soko zuri zaidi.
Naye mkimbiza mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Wazo Mwang’onda baada ya kuweka jiwe la msingi amemshukuru mwekezaji huyo kwakuweza kujenga kiwanda cha ubanguaji wa korosho kwani kitainua fursa za ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Zakia Saidi Mmoja wa wakulima wa korosho Kijiji cha Nyengedi amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa kimemaliza changamoto za korosho katika maeneo ya kusini pamoja na kupata fursa za ajira kwa wananchi wa Lindi.