
Dar es Salaam. Matumizi ya mitandao ya kijamii kupita kiasi, hali ngumu ya kiuchumi, changamoto za mahusiano ya kimapenzi, kutofanya vizuri katika masomo, shinikizo la maisha na matarajio makubwa, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, vimetajwa kuwa vichocheo vikuu vya matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa leo Mei 1, 2026 na wadau mbalimbali wa afya ya akili walioshiriki katika kongamano la uzinduzi wa kampeni ya ‘Kijana Tubonge’, ambayo imelenga kuwaleta pamoja vijana wa kuanzia umri wa miaka 15 hadi 35 kuwapa elimu itakayowasaidia kuongeza utambuzi juu ya umuhimu wa kulinda afya ya akili.
Akizungumza katika hafla ya kampeni hiyo iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Activista Tanzania, Edward Masele, amesema utafiti mdogo walioufanya hivi karibuni umebaini kuwa mambo hayo yamechangia baadhi ya vijana kujikuta wakipata tatizo la afya ya akili.
“Mfano kwa vijana wa vyuo vikuu asipofanya vizuri katika mitihani yake na kupata ‘sapu’ anaweza kujikuta akipata msongo wa mawazo akifikiria jinsi familia yake ilivyojinyima kumlipia ada, wakitarajia atafanya vizuri.
“Hali kadhalika, mahusiano ya kimapenzi yamekuwa changamoto haswa yanapoenda ndivyo sivyo, yanavuruga akili za vijana,” alisema Masele.
Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Tanzania Health Alliance, Mwanaasha Mkwizu amebainisha kuwa matumizi ya mitandao kupita kiasi yanaweza kuchangia kuathiri hali ya kujithamini, hususan vijana wanapojilinganisha na maisha ya wengine wanaowaona mitandaoni.
Amesema vijana wengi wanalazimisha maisha yaliyo nje ya uwezo wao kutokana na presha ya utandawazi na mitandao ya kijamii.
Pia, Mkwizu aligusia suala la matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii ambayo yanachangia ukatili wa kijinsia mitandaoni
“Vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii ndivyo sivyo. Globalization inaleta presha, video zinavuja, na taarifa binafsi kusambaa kunamfanya mtu achanganyikiwe,” ameeleza.
Kwa upande wake Ofisa Huduma, Imaculate Ibrahim kutoka Shirika la Green Conservers ameongeza kuwa hata mabadiliko ya tabianchi yanachangia tatizo la afya ya akili kwa vijana.
Ametolea mfano kijana aliyeamua kujiajiri kwa kufanya kilimo kisha mafuriko yakachukua mazao yote, hali inayompelekea kuingia kwenye msongo wa mawazo.
Nini kinapaswa kufanywa kwa vijana
Mkwizu amesisitiza kuwa daktari wa kwanza wa akili ya mtu ni yeye mwenyewe kwa kukubali uhalisia wa maisha badala ya kuishi kwa shinikizo.
Pia, amewasisitiza vijana wanapopitia changamoto za aina mbalimbali wasikae nazo tu wawe na utamaduni wa kuzungumza.
“Vijana wanapaswa kusema changamoto zinazowakabili kwa watu wanaowaamini ili kupunguza mlimbikizo wa mawazo unaoweza kupelekea maamuzi magumu kama kujidhuru,” amesema.
Kwa upande wake Masele ametoa wito kwa Serikali kuanzisha madawati ya ushauri wa kisaikolojia (counseling) katika kila chuo na shule ili kuwapa vijana nafasi ya kutoa machungu yao.
Pia, ameomba kuwezeshwa zaidi kwa wataalamu kufika maeneo ya vijijini ambako elimu ya afya ya akili inapatikana kwa uchache.