
Dodoma. Wakati Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo akihoji hatima ya mabando ya simu yanayobaki baada ya muda wa matumizi kuisha, wadau wa mawasiliano nchini walikosoa utaratibu huo wakisema ni tatizo la muda mrefu ambalo limeachwa bila ufumbuzi.
Shigongo alitoa kauli hiyo juzi bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aliitaka Tanzania kujifunza kutoka Afrika Kusini, ambako wamepitisha sheria inayoruhusu matumizi ya vifurushi kulingana na kiwango badala ya muda.
Mamlaka ya Mawasiliano ya Afrika Kusini (ICASA) imetangaza kanuni mpya zitakazoanza kutumika Januari 23, 2027, zikiwa na lengo la kuboresha haki za watumiaji.
Marekebisho hayo yanajulikana kama Kanuni za Marekebisho ya Hati ya Huduma kwa Mtumiaji na Msajili, 2025, na yanaleta mabadiliko makubwa katika matumizi ya vifurushi vya data, sauti na ujumbe mfupi (SMS).
Kwa mujibu wa ICASA, kampuni za simu zitalazimika kuruhusu mabaki ya vifurushi ambavyo havijatumika kuhamishwa angalau mara moja bila gharama, mradi laini ya mtumiaji itaendelea kuwa hai.
Hatua hii inalenga kupunguza hasara kwa watumiaji wanaoshindwa kumaliza vifurushi kabla ya muda kuisha.
Shigongo alisisitiza kuwa katika zama za uchumi wa kidijitali, ni ajabu kuona watu wanapoteza vifurushi walivyonunua kwa sababu ya muda.
“Sitaki kusema kama kuna wizi, lakini Watanzania wanajiuliza bando linapobaki linaenda wapi?” alihoji.
Aliongeza kuwa hata utaratibu wa kununua vifurushi vya muda una changamoto, kwani wakati mwingine muda haukamiliki au matumizi hayaendani na muda uliopangwa.
Alitolea mfano vifurushi vya televisheni akisema pale mteja anapolipia kwa mwezi mmoja, anatazama televisheni kwa siku zilezile 30, tofauti na ilivyo kwenye mawasiliano ya simu.
Pia alilalamikia mfumo wa kukatwa fedha moja kwa moja kwenye salio la kawaida pindi kifurushi kinapoisha bila ridhaa ya mtumiaji.
Kwa mujibu wa Shigongo, takwimu zinaonyesha asilimia 41 ya Watanzania wanatumia simu janja, asilimia 87 wanatumia simu kwa ujumla, huku watumiaji wa mitandao ya kijamii wakikaribia milioni 57. Licha ya ukuaji huo, malalamiko mengi yanahusu huduma za vifurushi.
“Simshtaki mtu hapa ila natimiza wajibu wangu wa kibunge. Zamani mahitaji ya msingi yalikuwa malazi, chakula na afya, lakini sasa data zimekuwa hitaji muhimu.”
Akifafanua zaidi kuhusu mfumo wa Afrika Kusini, alisema vifurushi vitatumika kwa kuzingatia muda wake, ambapo kifurushi chenye muda mfupi kitatumika kwanza, ili kuzuia upotevu.
Pia, watumiaji watapata taarifa za matumizi kupitia SMS wanapofikia asilimia 50, 80 na 100 ya matumizi.
Kanuni hizo pia zinakataza utozwaji wa gharama za ziada bila ridhaa ya mtumiaji, na kuruhusu uhamishaji wa vifurushi (data, dakika na SMS) kati ya watumiaji wa mtandao mmoja bila kikomo, isipokuwa vifurushi vya promosheni au vya muda mfupi.
Aidha, iwapo kutakuwa na hitilafu ya mtandao, muda wa kifurushi utaongezwa kufidia muda uliopotea.
Shigongo alipendekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Baraza la Watumiaji (TCRA CCC) ichunguze mifumo ya nchi nyingine kama Kenya, Uganda na Rwanda ili kuona uwezekano wa kuboresha huduma nchini.
Mbunge mwingine aliyechangia hoja ya bando ni wa Kilombero, Abubakar Asenga, aliyesema maumivu ya mabando ni makubwa, na Serikali inaweza kutazama na kuona jinsi ya kuyaondoa na makampuni ya simu yakabaki na faida.
Baada ya Shigongo na Asenga kutoa kauli hiyo, Spika wa Bunge, Mussa Zungu aliunga mkono hoja hiyo, akieleza kuwa suala hilo linaumiza wananchi na kuomba Serikali kulifanyia kazi.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki alisema Serikali imesikia malalamiko hayo na itaendelea kujadiliana na wadau ili kupata suluhisho, akisisitiza nia ni kuwaletea Watanzania unafuu.
Katika Bunge la 12, hoja ya gharama na ufanisi wa mabando iliwahi kujadiliwa na wabunge Mrisho Gambo, Ng’wasi Kamani na Miraj Mtaturu lakini bado imeendelea kubaki vitabuni bila utekelezaji.
Ilivyo Afrika Kusini
Mamlaka ya Mawasiliano ya Afrika Kusini (ICASA) imebainisha kuwa matumizi ya vifurushi yatafanywa kwa kuzingatia muda wa kuisha, ambapo kifurushi chenye muda mfupi zaidi ndicho kitakachotumika kwanza, lengo ni kuhakikisha kuwa hakuna kifurushi kinapotea bila sababu ya msingi.
Pia, kanuni zimeainisha kuwa katika kulinda zaidi watumiaji, watoa huduma watalazimika kutuma taarifa za matumizi kupitia SMS pale matumizi yanapofikia asilimia 50, 80 na 100.
Hata hivyo, watumiaji watapewa uhuru wa kuchagua kupokea au kutopokea taarifa hizo kulingana na mapendeleo yao.
Kanuni hizo pia zinazuia utozwaji wa gharama za ziada nje ya vifurushi bila ridhaa ya mtumiaji.
Hii ina maana kuwa mtumiaji hatatozwa viwango vya juu vya “out-of-bundle” isipokuwa kama atachagua mwenyewe kuingia kwenye mfumo huo.
Katika hatua nyingine muhimu, ICASA imeelekeza kuwa watumiaji waruhusiwe kuhamisha salio la vifurushi vyao, iwe ni data, dakika za maongezi au SMS kwa watumiaji wengine ndani ya mtandao huo huo, bila kikomo cha idadi ya uhamisho.
Hata hivyo, vifurushi vya promosheni, bure au vile vya muda mfupi (siku saba au chini) havitahusishwa na utaratibu huu.
Pia, iwapo mtumiaji atashindwa kutumia kifurushi chake kutokana na hitilafu ya mtandao, muda wa matumizi utaongezwa kulingana na kipindi kilichopotea.
Kilio cha wadau
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rukia Ambrose alisema mabadiliko hayo yanawezekana na hayataathiri faida za kampuni.
Alibainisha kuwa mfumo wa sasa unaumiza watumiaji, hasa wanafunzi wanaotegemea intaneti kwa masomo.
Mchambuzi wa uchumi, Magabilo Masambu alisema ni muhimu Serikali kuweka sera mpya zitakazolinda watumiaji.
Alipendekeza vifurushi visipotee kwa sababu ya muda kuisha bali viendelee hadi vitumike kikamilifu.
Aliongeza kuwa kampuni zinapaswa kutoa taarifa wazi kuhusu matumizi na masharti ya vifurushi, huku ushindani wa haki sokoni ukilazimisha maboresho ya huduma.
“Ninaona Serikali ya Tanzania kupitia mamlaka husika inapaswa kuweka sera mpya itakayolinda haki za watumiaji wa huduma za mawasiliano, ili watumiaji wakishanunua vifurushi, bando lisipotee kwa sababu ya muda kuisha bali liendelee kubaki hadi pale litakapomalizika kwa matumizi halisi.
Alisema hiyo itasaidia kuondoa malalamiko ya wananchi kupoteza fedha zao bila kupata huduma waliyonunua.
“Kampuni ziwajibike kutoa taarifa wazi kuhusu matumizi, salio na masharti ya vifurushi bila kuficha taarifa muhimu zinazoweza kuwaumiza wateja,” alisema na kuongeza.
“Serikali iweke kanuni zitakazozuia vifurushi kuisha kienyeji wakati mtumiaji hajavitumia, sawa na bidhaa nyingine ambapo mnunuzi hupata thamani kamili ya fedha yake.
Masambu amesisitiza kuwa ushindani wa haki sokoni ukiwapo utazilazimisha kampuni kuboresha huduma badala ya kuongeza mapato kupitia vifurushi vinavyoisha kabla ya matumizi.
“Wananchi wakitumia intaneti wakiwa wengi kwa uhakika kutaongeza ushiriki kwenye biashara mtandao, elimu ya kidijitali na huduma za Serikali mtandao,” alisema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kijamii Noel Shao alisema malalamiko hayo ni ya muda mrefu na yanahitaji hatua za haraka.
“Haiwezekani unanunua kifurushi cha mwezi kinaisha ndani ya siku moja. Hapa kuna walakini,” aliongeza.
Alisisitiza kuwa ni wakati wa Serikali kufanya marekebisho ya sheria ili kulinda watumiaji na kuondoa mfumo unaowaumiza wananchi.
“Hiki ni kilio cha muda mrefu haiwezekani unanunua kifurushi cha mwezi kinaisha ndani ya siku moja huku ni kuumiza wananchi, kama umenunua huduma ya mwezi basi kitumike ndani ya muda huo tofauti na hapo kuna walakini,” alisema.
Shao alisema ni muhimu Serikali kuangalia marekebisho ya sheria yatakayomwondolea mwananchi ukandamizwaji kwenye huduma.
Ukiacha hao, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi Oscar Mkude alisema hoja ya watu kununua vifurushi na kulazimishwa kuisha ndani ya muda fulani linapaswa kuangaliwa.
“Nimenunua kifurushi changu kama hakijaisha ndani ya muda basi niongezewe muda hadi uishe kwa sababu hii haimzuii mfanyabiashara kupata faida,” alisema.
Mkude alisema kwa upande wa mtu kununua kifurushi na kuisha kwa muda mfupi ni sawa, kutokana na matumizi yake kuwa makubwa.
Alisema katika hilo, kabla Serikali haijachukua hatua yoyote inapaswa kufanya utafiti, kwa kuwa lengo ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara kwa wafanyabiashara.