
Mikoani. Wakati nauli zikipanda leo Mei Mosi, baadhi ya wananchi wameonyesha hisia tofauti kuhusu mabadiliko hayo, wengi wakilalamikia kuongezeka kwa gharama za maisha na wengine wakiona ni hatua isiyoepukika kutokana na hali ya uchumi.
Hatua hiyo inafuatia tangazo la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) la kuongeza nauli za mabasi ya masafa marefu na daladala, likieleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuendana na kupanda kwa bei ya mafuta pamoja na gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamesema ongezeko hilo linaongeza ugumu wa maisha kwao hasa kwa wale wanaotegemea usafiri wa umma katika shughuli za kila siku, huku wengine wakisisitiza kuwa linapaswa kuendana na uhalisia wa kipato cha wananchi.
Kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, nauli kutoka Bariadi kwenda Dar es Salaam imeongezeka kutoka Sh85,000 hadi Sh 95,000, huku ile ya kutoka Bariadi kwenda Arusha ikipanda kutoka Sh50,000 hadi kufikia 60,000.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa ongezeko hilo linawaathiri moja kwa moja, hasa kwa wale wanaotegemea usafiri huo kwa shughuli za biashara na huduma za kijamii.
“Mimi nafanya biashara ndogo ndogo, hii nauli mpya imeniumiza sana. Inamaanisha gharama zangu zote zitapanda,” amesema David John wa mjini Bariadi.
Naye Neema Ruben amesema kuwa, licha ya kupanda kwa gharama za mafuta, bado mamlaka zinapaswa kuangalia masilahi ya wananchi wa kipato cha chini.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha daladala jijini Mbeya, Baraka Yusuph amesema wameanza matumizi ya nauli mpya kuanzia Mei 1, wakipandisha kuanzia Sh700 hadi Sh1,000 kulingana na umbali.
Amewataka madereva wote kuzingatia utaratibu uliowekwa na Serikali kwa kutozidisha kiwango hicho akiwaomba wananchi kutoa taarifa pale watakapoona wanaonewa kwa kupandishiwa nauli.
“Sisi pia viongozi tutafuatilia wale watakaozidisha kiwango hiki kwa kuchukua hatua, lakini pia mamlaka zikiwakamata hatutahusika kwa kuwa tumetoa utaratibu, wananchi watoe taarifa” amesema Yusuph.
Hata hivyo, nauli za bajaji zilianza kupanda kabla ya Mei Mosi, ambapo abiria hutumia Sh1,000 badala ya Sh800 zilizokuwa zikitumika hapo awali tangu bei ya mafuta ilipopanda na kuleta changamoto kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi jijini Mbeya, Vaileth Masanja amesema wameshazoea kulipa Sh1000 kwa kituo kwa usafiri wa bajaji sawa na daladala kutoka stendi kuu hadi Uyole na Nsalaga.
“Mbona nauli zilipanda muda mrefu, labda leo ndio wanazindua rasmi ila sisi wananchi tulishazoea Sh1,000 kwa kila kituo sawa na daladala kutoka mjini kwenda Nsalaga au Uyole kule Igawilo” amesema Vaileth.
Katika Mkoa wa Arusha uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kiwango cha nauli kimeendelea kubaki kilekile kilichopangwa na waendeshaji wa magari ya mizunguko ya mjini maarufu daladala isipokua barabara ya Kilombero hadi Usa River ambako nauli imekua Sh1,000 kutoka Sh900 ya awali.
Mabasi aina ya Coaster yameendelea kutoza kiasi cha Sh1,500 bila kujali umbali ambao abiria anaenda.
Mkazi wa Olasiti jijini hapa, Fatuma Ally amesema ametumia nauli ya Sh1,000 kufika Soko la Kilombero badala ya nauli mpya ambayo inapaswa kuwa Sh700.
“Kutoka Olasiti kuja Kilombero ni Sh1,000 nimeshuka Matejoo kuchukua mahindi ya kuchoma kutoka hapo hadi hapa ni Sh1,500 nikirudi nyumbani jumla nitakua nimetumia Sh3,500 hapo bado mambo mengine ya maisha,” amesema Fatuma.
“Kiukweli nauli zimeongezeka na zinazidi kufanya maisha yawe ghali, tuna familia na kila siku tunalazimika kupanda daladala kwenda kazini na kurudi, tunafanya kazi lakini kiasi kikubwa cha fedha kinaishia njiani,” amesema.
Pia, barabara ya Kilombero kwenda Njiro nauli mpya inapaswa kuwa Sh800, lakini abiria wameendelea kutozwa Sh1,000.
Mkazi wa eneo la Intel, John Mollel amelalamikia magari yaliyopewa leseni ya kufanya safari zake kutoka Soko la Kilombero hadi Mapambazuko wakati jioni kukatisha safari kuishia eneo la Dampo kwa lengo la kujipatia mapato zaidi na kuiomba Latra kuingilia kati.
Kwa upande wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, hivi sasa nauli kutoka mji mdogo wa Orkesumet hadi jijini Arusha imepanda kutoka Sh15,000 hadi Sh20,000 na kutoka Orkesumet hadi mji mdogo wa Mirerani imetoka pia Sh15,000 hadi Sh20,000.
Pia, nauli imepanda kutoka mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro hadi njia panda ya Moshi na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000 umbali wa kilomita 26.
Mkazi wa kata ya Orkesumet, Julius Mollel amesema wamiliki wa mabasi hawapaswi kulaumiwa nauli za mabasi kupanda kwani bei ya nishati ya mafuta imepanda hivyo nauli nazo zitapanda.
“Huwezi kuendelea na kutoza nauli ile ile kwa sehemu moja ili hali mafuta yamepanda bei na pia barabara nazo zimeharibika na mvua na kusababisha wamiliki wa magari kuhofia kuharibika magari yao,” amesema Mollel.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wameonesha kulipa nauli hiyo kwa shingo upande huku wachache wakiomba nauli za wanafunzi zibaki kama zilivyokuwa awali.
Mmoja wa abiria kutoka Kihonda Azimio, Musa Joram amesema nauli hiyo mpya iliyotangazwa na Latra tayari ilishaanza kutozwa wiki mbili zilizopita hata hivyo wapo baadhi wamekuwa wameonekana kushindwa kumudu nauli hiyo na wengine wakiridhika.
“Sisi wananchi wa Manispaa ya Morogoro hii nauli ya Sh800 iliyotangazwa na Latra hatuoni kama ni mpya maana tulishaanza kulipishwa hata kabla haijatangazwa, na sisi kutokana na shida ya usafiri tulilazimika kutoa,” amesema Jaram.
Hata hivyo, ameiomba Latra kutopandisha nauli Kwa wanafunzi na kuiacha iwe ile ile ya Sh200 kwani amesema kuwa kufanya hivyo kutapunguza gharama na mzigo kwa wazazi hasa wale wenye mtoto zaidi ya mmoja wanaosoma.
“Mwanafunzi hana chanzo chochote cha mapato anategemea apate nauli kutoka Kwa mzazi, mzazi naye akipanda daladala kwenda kutafuta rizki analipa nauli ya Sh800, linaloumiza zaidi unakuta mzazi anawatoto wawili ama watatu ambao licha ya kuwapa nauli, lakini pia anapaswa kuwapa hela ya kula shule,” ameeleza Joram.
Flora Msangi mkazi wa Kihonda maghorofani, ameiomba Latra na mamlaka nyingine zinazosimamia usafiri wa ardhini hususani daladala kuwachukulia hatua kali madereva wanaokatisha safari na kuhamiasha abiria kwenye daladala nyingine kwani amesema kuwa kitendo hicho kinasababisha ufumbufu mkubwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha madereva wa daladala Manispaa ya Morogoro, Isaa Rusogo amesema tangu asubuhi ya leo, hajapata malalamiko kutoka kwa madereva wala abiria kuhusu nauli mpya ya Sh800 na hiyo ni ishara kwamba abiria wameipokea na kuikubali.
Mkoani Shinyanga, baadhi ya wananchi wameonyesha kutokukubaliana na kupanda wa nauli sababu ya hali ya kimaisha ya mkoa huo na shughuli zote za kiuchumi.
Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Shija Bundara ameeleza kuwa, hakuna mzunguko mkubwa wa pesa hasa kwa wananchi wa kipato cha chini.
“Gharama hizi zimekuja katika kipindi ambacho sio kizuri, kwa sababu hakuna mvua ambazo zingechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao, ambapo inapelekea kutokuwa na mzunguko mkubwa wa pesa hasa kwa wananchi wa kiwango cha chini,” amesema Bundara.
Kwa upande wake Neema Nkilijiwa ameeleza kuwa, “Katika utekelezaji wa nauli mpya basi wangeangalia ni watu wa kiwango gani cha uchumi wanawahudumia, ndio waweke kiwango cha nauli hasa hizi daladala, kwa sababu nauli hizi zinafanya na gharama za maisha kupanda kwa sababu kila kitu kinategemea usafirishaji” amesema Neema.
(Imeandikwa na Samwel Mwanga (Simiyu), Sadam Sadick (Mbeya), Joseph Lymo (Simanjiro), Filbert Rweyemamu (Arusha) na Hellen Mdinda (Shinyanga)