Dar es Salaam. Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku ikisisitiza umuhimu wa elimu endelevu kwa watumiaji ili kuhakikisha wanatumia nishati hiyo kwa usahihi na usalama.

Akizungumza jana Alhamis Aprili 30, 2026 wakati wa ufunguzi wa duka maalum la Oryx Gas lililopo eneo la Banana jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko na Mauzo, Shaban Fundi, amesema kampuni hiyo imejipanga kusogeza huduma karibu na wananchi sambamba na kutoa elimu ya matumizi bora ya gesi.

“Tumeunganisha nguvu zetu kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia Watanzania wote. Tunatambua lengo la Serikali la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2030,” amesema Fundi.

Ameongeza kuwa maduka hayo maalum yatatumika pia kutoa elimu ya matumizi salama ya gesi, akibainisha kuwa changamoto nyingi za watumiaji hutokana na uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya mitungi ya gesi.

“Kutumia gesi siyo tu kuipata, bali ni kuijua. Wapo wanaoona kama ni ghali au inaisha haraka, kumbe ni matumizi yasiyo sahihi kama kufungua na kufunga mitungi,” amesema.

Fundi amesema kupitia huduma mpya ya usambazaji, wateja hawatalazimika kubeba mitungi, badala yake wataituma kampuni namba zao na gesi itawafikishwa walipo bila gharama za ziada.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NASSCO, Tarik Nassoro, ambaye ni mshirika wa Oryx Gas, amesema kampuni hizo zinaendelea kufungua maduka katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Wilaya ya Ilala, huku akiwataka Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Naye Baba Lishe, Dickson Kuga na Mama Lishe, Beatrice Shayo wamesema matumizi ya nishati safi yamekuwa msaada mkubwa kwa mama na baba lishe, wakibainisha kuwa gesi inaokoa muda na haina madhara ya kiafya kama ilivyo kwa nishati za asili.

“Gesi imerahisisha kazi yetu, tunaokoa muda na pia tunahakikisha afya zetu zinakuwa salama,” wamesema.

Oryx Gas imesema tayari ina maduka zaidi ya 1,000 nchini na inaendelea kupanua mtandao wake ili kuhakikisha huduma ya nishati safi inawafikia Watanzania wengi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *