Kahama. Uwepo wa kampuni bubu za ulinzi wilayani Kahama mkoani Shinyanga kunaelezwa kuendelea kuchochea uhalifu katika maeneo mbalimbali wakati ambapo jeshi la polisi likipambana kuhakikisha ulinzi wa wananchi na mali zao unaimarika.

Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, ameyasema hayo Aprili 30, 2026, wakati akipokea jengo la polisi jamii na la operesheni na mafunzo lililojengwa na wadau wa ulinzi wilayani Kahama.

Jengo hilo limejengwa kwa nguvu za wadau wa ulinzi kwa zaidi ya asilimia 90, limegharimu zaidi ya Sh25 milioni ikiwa ni matokeo ya ushirikishwaji wa wananchi kupitia dhana ya polisi jamii.

Akizungumzia kampuni hizo, Magomi amesema jeshi hilo kupitia kitengo cha polisi jamii linaendelea kufuatilia kampuni zote za ulinzi binafsi kuhakikisha zinajisajili kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni zilizopo.

Askari wa jeshi la polisi wilaya ya Kahama pamoja na wananchi wakiwa katika uzinduzi wa jengo la polisi jamii na la operesheni na mafunzo wilaya ya Kahama lilijengwa na wadau wa ulinzi wilayani humo.

Amesema wanaendelea na jitihada za kukomesha Kampuni hizo ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao, na hata kwa kampuni zilizopata vibali lakini zinakiuka taratibu pia zitafutwa.

Ametaja athari za kampuni hizo kuwa ni pamoja na kutumia walinzi wasio na mafunzo hali inayochochea uhalifu.

Amesema “Tunaendelea kuzisaka hizi kampuni, kuhakikisha zinafuata sheria taratibu na kanuni. Uwepo wa kampuni bubu ni chanzo cha uhalifu, msako ulishaanza na unaendelea ili zifutwe”

Kauli ya RPC Magomi inafuatia ombi la mwenyekiti wa kampuni binafsi wilayani Kahama Fabian Marius kwa jeshi hilo kudhibiti kampuni hizo zinazochafua taswira ya kampuni binafsi za ulinzi.

Amesema uwepo wa kampuni hizo unaathiri utendaji wa kampuni binafsi za ulinzi wilayani humo, ikiwemo malipo stahiki ya watumishi kulingana na maelekezo ya serikali.

Amesema, “Kampuni zile za uchochoroni bado zipo, zinaturudisha nyuma kimaendeleo, tulijitengenezea utaratibu wa bei elekezi kwa kuzingatia kima cha chini cha serikali, lakini kampuni hizi bubu zimekuwa zikipita juu kwa juu na kuchukua malindo kwa bei ndogo.”

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, mwenyekiti wa wafanyabiashara wilaya ya Kahama Charles Machali amesema, wamefikia hatua ya ujenzi wa jengo hilo, ili kuunga mkono juhudi za jeshi hilo katika kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao.

Amesema, “Sisi kama wafanyabiashara tuko tayari kuendelea kuliunga mkono jeshi letu, kutokana na matunda tunayoyaona ya usalama kwenye biashara na maeneo yetu ya makazi.”

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi wa pili kushoto akiongoza zoezi la uzinduzi wa jengo la polisi jamii na la operesheni na mafunzo wilaya ya Kahama. Picha na Amina Mbwambo

Wilaya ya Kahama ina kampuni binafsi za ulinzi 51, huku bado kukielezwa kuwa na changamoto ya kampuni bubu.

Hata hivyo ujenzi wa jengo hilo na matokeo ya ushirikishwaji wa wananchi katika masuala yanayohusu ulinzi na usalama kupitia polisi jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *