Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ametangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara kutoka Sh300,000 hadi Sh500,000 kwa mwezi.

Dk Mwinyi ametangaza kima hicho leo Mei 1, 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema mshahara huo mpya utaanza kutumika kuanzia Januari 2027, akibainisha kuwa uamuzi huo umezingatia hali ya uchumi wa nchi, ongezeko la gharama za maisha pamoja na dhamira ya Serikali ya kuongeza motisha kwa wafanyakazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati,” amesema Dk Mwinyi, akiwataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uzalendo ili kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Aidha, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, na itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *