
Dar es Salaam. Ni sababu ya kujiamini, mvuto wa kipekee na ishara ya mitindo ya kisasa, lakini nyuma ya uzuri huo wa viatu virefu maarufu kama ‘high heels’, kuna hatari kubwa inayowanyemelea wavaaji wa viatu hivyo kwa muda mrefu.
Katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya mijini, si jambo la ajabu kuona wanawake wakitembea kwa maringo na kujiamini wakiwa wamevaa viatu virefu, iwe ni kazini, kwenye sherehe au katika shughuli za kijamii.
Kulingana na utafiti uliochapishwa kwenye tovuti ya Physio-Pedia, matumizi ya mara kwa mara ya viatu hivyo hubadilisha kabisa mfumo wa mwili na namna unavyofanya kazi na kusababisha madhara kwa mvaaji.
Kilichoelezwa kwenye utafiti huo kinashabihiana kwa kiasi kikubwa na simulizi ya Asha Mwakabonga, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ambaye alijikuta akiingia kwenye mfululizo wa maumivu bila kutambua chanzo halisi mapema.
Kwa Asha, yote yalianza kama maumivu madogo ya nyayo yaliyokuwa yakijitokeza mara chache baada ya kutoka kazini. Hakuyapa uzito mkubwa, akidhani ni uchovu wa kawaida unaotokana na majukumu ya kila siku.
Hata hivyo, kadri muda ulivyokuwa ukisonga, maumivu hayo yalianza kuwa ya mara kwa mara na baadaye kuenea hadi kwenye vifundo vya miguu na hatimaye mgongoni.
Asha amesema katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, alikuwa amezoea kuvaa viatu virefu karibu kila siku alipokuwa akienda kazini, akiamini vinamfanya aonekane nadhifu, mwenye mvuto na kujiamini zaidi mbele ya wateja na wafanyakazi wenzake.
“Kwa kazi yangu, nilihisi mwonekano ni muhimu sana, hivyo viatu virefu vilikuwa sehemu ya lazima ya mavazi yangu ya kila siku,” amesema.
Amesimulia kuwa kulikuwa na nyakati alihisi maumivu makali, lakini aliendelea kuvumilia akiamini ni hali ya kupita.
Wakati mwingine alilazimika kubeba dawa za kupunguza maumivu ili kuweza kumudu siku yake ya kazi, bila kufikiria athari za muda mrefu.
“Nilifikiri ni uchovu wa kawaida tu, lakini baadaye nilishindwa hata kusimama muda mrefu. Hali ilipofika hapo ndipo nilipoamua kwenda hospitali kwa uchunguzi zaidi,” amesema.
Baada ya kufanyiwa vipimo, madaktari walibaini kuwa matumizi ya muda mrefu ya viatu virefu yalikuwa yamesababisha athari katika mfumo wa mifupa na misuli, hasa kwenye nyayo na mgongo.
Taarifa hiyo ilimlazimu kubadili kabisa mtindo wake wa maisha.
“Sasa nimepunguza kabisa matumizi ya viatu virefu. Navaa mara chache sana na kwa muda mfupi. Kwa sasa niko kwenye matibabu ya mgongo na mazoezi maalumu ya kurekebisha hali yangu,” ameeleza.
Hali inayofanana na iliyompata pia mfanyabiashara wa nguo Kariakoo, Rehema Said ambaye amesema alipata jeraha la kifundo cha mguu baada ya kujikwaa akiwa amevaa viatu virefu harusini.
“Ilikuwa bahati mbaya, lakini daktari alinieleza kuwa viatu virefu vinapunguza uthabiti wa mwili. Tangu siku hiyo, nimekuwa mwangalifu sana,” amesema Rehema.
Uchambuzi wa kitaalamu uliofanywa na Physio-Pedia umeonyesha kuvaa viatu virefu husogeza uzito wa mwili mbele na kubadilisha mkao wa asili wa mwili, jambo linaloathiri mgongo, shingo na hata kichwa.
Akizungumzia na Mwananchi daktari bingwa wa mifupa na viungo, Joseph Mhando amesema mabadiliko hayo ya mkao ndiyo chanzo kikuu cha maumivu ya mgongo kwa wanawake wengi wanaovaa viatu hivyo kwa muda mrefu.
Amesema wanawake wengi wanaowafikia hospitalini hukiri kutumia viatu virefu kwa muda mrefu bila kujua madhara yake.
“Tunapokea wagonjwa wengi wenye maumivu ya mgongo na magoti, na ukiwauliza historia yao unakuta wamezoea kuvaa viatu virefu kila siku. Tatizo si siku moja au mbili matumizi ya muda mrefu,”.
Amesema tafiti zinaonyesha kuwa hali hiyo husababisha mgongo wa chini kupinda zaidi, jambo linaloweza kuleta maumivu ya muda mrefu na hata ulemavu wa kudumu iwapo halitadhibitiwa.
Mbali na mgongo, viatu virefu vinaathiri pia namna mtu anavyotembea, utafiti unaonyesha kuwa kutembea kwa viatu hivyo hupunguza ufanisi wa mwendo na kuongeza uchovu wa misuli kwa kasi kubwa zaidi.
“Kwa mujibu wa wataalamu, mabadiliko hayo huanza pale kisigino kinapoinuliwa na kulazimisha mwili kusogea mbele, ili kudumisha usawa, hali hiyo huongeza mzigo kwenye mgongo wa chini na magoti,” amesema Dk Mhando.
Mtaalamu wa tiba viungo Dk Neema Komba amesema mabadiliko hayo huathiri moja kwa moja misuli ya mwili na uwezo wa mtu kujimudu kimwili.
“Unapoinua kisigino, mwili hulazimika kujirekebisha ili kudumisha usawa. Hapo ndipo mgongo wa chini unapobeba mzigo mkubwa zaidi kuliko kawaida. Misuli inalazimika kufanya kazi ya ziada ili kudhibiti mwili.
“Hii husababisha uchovu, kupungua kwa nguvu na wakati mwingine kuongeza hatari ya kuanguka au kupata majeraha. Viatu virefu huongeza shinikizo kwenye viungo hivyo, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa viungo (osteoarthritis) kwa muda mrefu” amesema Dk Komba.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Foot and Ankle Research umebainisha kuwa matumizi ya viatu virefu husababisha mabadiliko katika mwili kuanzia mgongo hadi vidole vya miguu, hali inayochangia maumivu ya viungo na majeraha ya mara kwa mara.
Athari hizo haziishii hapo amesema sehemu ya mbele ya mguu ndiyo inayopata mzigo mkubwa zaidi wakati wa kuvaa viatu virefu, hali inayosababisha matatizo kama vile kuvimba kwa kidole kikubwa, maumivu ya nyayo na mabadiliko ya muundo wa vidole.
“Vidole vinabanwa mbele ya kiatu, hasa kama ni chembamba. Hii inaweza kusababisha ulemavu wa kudumu wa mguu,” amesema Dk Komba.
Mtaalamu huyo amebainisha kuwa presha kubwa inayowekwa kwenye mguu inaweza pia kuongeza hatari ya majeraha ya kifundo cha mguu na kupoteza usawa wa mwili, hasa kwa viatu vyenye visigino virefu na vyembamba.
Hata hivyo, pamoja na tahadhari hizo, Dk Mhando amekiri kuwa si rahisi kwa wanawake wengi kuacha kabisa kuvaa viatu virefu kutokana na sababu za kijamii na kiutamaduni, ikiwemo mwonekano na kujiamini.
“Hatusemi wanawake waache kabisa kuvaa viatu virefu, lakini ni muhimu kujua namna ya kupunguza madhara yake. Urembo ni muhimu, lakini afya ni muhimu zaidi. Ni vyema kufanya maamuzi ya mavazi yanayolinda mwili kwa muda mrefu,” amesema Dk Mhando.
Ameshauri wanawake kuchagua viatu vyenye visigino vifupi kati ya sentimita 3 hadi 5, ambavyo vinaelezwa kuwa salama zaidi kwa kudumisha usawa wa mwili.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuchagua viatu vyenye kisigino kipana ili kuongeza uthabiti na kupunguza hatari ya kuumia, pamoja na kutumia vifaa maalumu vya ndani ya kiatu ili kupunguza presha kwenye mguu.
Katika hilo, Dk Mhando anashauri wanawake kubadilisha viatu mara kwa mara, kuepuka kusimama au kutembea kwa muda mrefu wakiwa wamevaa viatu virefu, na kufanya mazoezi ya kunyoosha misuli ili kuondoa mkazo unaotokana na matumizi ya viatu hivyo.