OFISA Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema timu hiyo ipo tayari kwa mchezo wa Jumapili, wiki hii, dhidi ya Yanga akisisitiza kuwa ushindi ndio silaha pekee ya kudumisha furaha kwa mashabiki wa Msimbazi.

Kauli hiyo ameitoa leo, Ijumaa, ikiwa ni siku chache baada ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye fainali ya Muungano, bao lililofungwa na Seleman Mwalimu Jumatano iliyopita.

Akizungumza kuelekea mchezo wa Jumapili ambapo utapigwa Kwenye Uwanja wa  Meja Jenerali Isamuhyo, Ahmed amesema ushindi huo umeongeza presha kuelekea dabi hiyo huku kila timu ikisaka matokeo chanya.

SIMBA 09

“Tumempasua kwa hiyo na yeye anataka ushindi ili kufuta kilichotokea Zanzibar. Sisi hatupo tayari kuruhusu hilo. Simba furaha yetu idumu kwa siku tatu na njia pekee ya kuifanya idumu ni kushinda,” amesema.

Ameongeza kuwa muda mfupi kati ya mechi mbili hizo unaifanya dabi hiyo kuwa ya kipekee na yenye ushindani mkubwa zaidi.

“Tungekuwa tumemfunga miezi mitatu au minne iliyopita, presha isingekuwa kubwa. Lakini tumemfunga Jumatano, leo ni Ijumaa na mechi ni Jumapili. Hii ni mechi ngumu sana,” amesema.

Katika msimamo wa ligi, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 47 huku Simba ikifuatia na pointi 42, hali inayoongeza uzito wa mechi hiyo  ya Jumapili.

SIMBA 08

Ahmed pia amesisitiza dhamira ya Simba kurejesha heshima yake msimu huu.

“Wao walichukua Mapinduzi, sisi tumechukua Muungano. Zanzibar tumegawana, sasa ni muda wa Bara. Tunataka kufanya vizuri kwenye ligi na Kombe la Shirikisho lengo ni kubeba yote au kugawana.”

Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba umetangaza rasmi viingilio vya mechi hiyo, huku ukichukua hatua za kudhibiti ulanguzi wa tiketi. Tiketi zimeanza kuuzwa rasmi na mashabiki wamehimizwa kununua mapema kuelekea dabi hiyo kubwa ya watani wa jadi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *