
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amekejeli mzingiro wa jeshi la majini la Marekani dhidi ya Iran, akieleza kuwa mipaka mirefu ya nchi hiyo inabatilisha jaribio lolote la kuizingira Jamhuri ya Kiislamu.
Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa X, Qalibaf amependekeza hali ya kidhahania na ya kufikirika tu ambapo kuta mbili zimejengwa kote Marekani; mmoja kutoka Jiji la New York hadi Pwani ya Magharibi na mwingine kutoka Los Angeles hadi Pwani ya Mashariki.
“Ukijenga kuta mbili, mmoja kutoka NYC hadi Pwani ya Magharibi na mwingine kutoka LA hadi Pwani ya Mashariki, urefu wa jumla utakuwa kilomita 7,755, ambao bado ni mfupi zaidi kwa karibu kilomita 1,000 ukilinganisha na mipaka jumla ya Iran,” ameandika Qalibaf.
Mohammad Qalibafu amemkejeli Waziri wa Vita wa Marekani kwa kuandika: “Kila la heri kuizingira nchi iliyo na mipaka yenye urefu huo!”
Spika wa Bunge la Iran ameongeza angalizo kwa Waziri wa Vita wa Merekani Pete Hegseth, ambaye siku ya Alhamisi alitetea mzingiro wa baharini dhidi ya Iran mbele ya wajumbe wa Kongresi na kuandika: “Angalizo kwa Pete Hegseth: 1 km = 0.62 maili.”
Marekani imeweka mzingiro wa majini dhidi ya bandari za Iran kufuatia vita vya kichokozi vya nchi hiyo na Israel tarehe 28 Februari.
Ikumbukwe kuwa, jumla ya mipaka ya nchi kavu na bahari ya Iran ina urefu wa kilomita 8,700, ikijumuisha mwambao wa Ghuba ya Uajemi, Ghuba ya Oman na Bahari ya Caspian.