
Mufti Mkuu na Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu wa Russia ameeleza kuwa, Umma wa Kiislamu unapaswa kusimama pamoja na Iran dhidi ya njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na akasema: “Iwapo Waislamu watakuwa na umoja na mshikamano, kambi ya shetani haiwezi kamwe kurudia uchokozi dhidi ya Gaza, Syria, Iran na Lebanon.”
Akizungumza katika kikao chake na Balozi wa Iran mjini Moscow, Mufti Sheikh Ravil Gaynutdin ametoa shukurani zake kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wema wake kwa Baraza la Mufti wa Russia na maombi na dua zake kwa ajili ya Waislamu wa nchi hiyo.
Mufti Mkuu wa Russia ametangaza tena mshikamano wa Waislamu wa nchi hiyo na serikali na wananchi wa Iran dhidi ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni na Marekani.
Amesema: Waislamu wa Russia wanaiunga mkono Iran na wanashangazwa na uvumilivu na ujasiri wa taifa la Iran. Mufti Gaynutdin ameongeza kuwa: “Wavamizi walikuwa na nia ya kuwachochea wananchi dhidi ya serikali kwa kuikalia kwa mabavu Iran, lakini taifa la Iran limevuruga mipango hiyo miovu kwa umoja na mshikamano wake.”
Mkuu wa Baraza la Mufti wa Shirikisho la Russia amesema njama za utawala wa Kizayuni na Marekani ni kuzigombanisha nchi za Kiarabu na Iran na kuibua mpasuko baina ya Umma wa Kiislamu na kuongeza: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kwa uaminifu na uwazi kwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kupitia jamii ya kimataifa kwamba iwapo itashambuliwa kutoka katika kambi za kijeshi za Marekani zilizoko katika nchi hizo, Iran italazimika kujibu kwa kushambulia kambi hizo.
Mufti Gaynutdin amesema: “Kambi za kijeshi za Marekani haziwezi kuhakikisha usalama na utulivu, na nchi za Kiarabu zimetambua jambo hilo.”
Mkuu wa Utawala wa Kidini wa Kiislamu wa Russia amesema kuwa, kukaliwa kwa mabavu ardhi za Kiislamu na utawala wa Kizayuni ni changamoto kubwa kwa Umma wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: “Njia ya Umma kukabiliana na njama hizo ni umoja, mshikamano na udugu.”