
Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu, ametoa wito kwa Ulaya kuchukua hatua za haraka baada ya utawala ghasibu wa Israel kuzuia na kukamata meli za misaada ya kibinadamu zinazojulikana kama Samood Flotilla zilizokuwa zikielekea Ukanda wa Gaza huko Palestina kwa ajili ya kuvunja mzingio wa kikatili wa utawala huo.
Francesca Albanese ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za Ulaya baada ya jeshi la wanamaji la Israel kukamata meli za Global Solidarity Fleet katika bahari ya kimataifa karibu na pwani ya Ugiriki.
Albanese amesema: “Kukamatwa meli hizo katika maji ya kimataifa ni tukio hatari ambalo linalazimu radiamali kubwa katika bara la Ulaya.”
Ameongeza kwa kusema: “Kuruhusu kushambuliwa meli katika maji ya kimataifa karibu na Ulaya kunazua maswali mazito kuhusu kiwango cha kuheshimiwa sheria za kimataifa.”
Vilevile Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maeneo ya Palestina amesisitiza kuwa, kwa kutilia maanani tuhuma zinazotolewa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kwa ukiukaji mkubwa wa sheria katika ardhi za Palestina, kuendelea vitendo hivyo kunaweza kusababisha mshtuko mkubwa katika duru za Ulaya.
Msafara wa misaada ya kibinadamu wa meli za Samood Flotilla, ambao umeshambuliwa na utawala wa Israel, unatambuliwa kuwa mojawapo ya harakati kubwa zaidi za majini za raia za kuunga mkono na kuwatetea Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Msafara huo uliozinduliwa Aprili 12, unahusisha zaidi ya meli na boti 100 kutoka bandari mbalimbali za Uhispania, Italia na Tunisia. Takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya meli 30 za msafara huo, tisa zinafanya kazi chini ya bendera ya Uhispania.
Samood Flotilla ilianzishwa kwa lengo la kuvunja mzingiro wa majini wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Malengo makuu ya operesheni hiyo ni kutoa misaada ya kibinadamu, kuanzisha kivuko cha bahari cha kiraia hadi Gaza, na kusaidia juhudi za misaada na ujenzi mpya wa eneo hilo lililoharibiwa na jeshi katili la Israel.