Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohi El-Din Salem, amefichua kwamba serikali ya nchi yake itafanya tathmini ya uhusiano wake wa kimataifa na kikanda baada ya vita, na hautakuwa sawa na hapo awali. Amesema kuwa wizara yake imezuia majaribio ya kulazimisha masuluhisho ya kigeni kwa nchi yake na haitakubali mashinikizo ya aina yoyote.

Salem amesema kwamba nchi na mashirika mbalimbali yalitumia kiasi kikubwa cha fedha kulazimisha masuluhisho ya kigeni kwa Sudan, na wengine walituma wajumbe na wawakilishi kutoa mashinikizo ya kukubali masuluhisho hayo, lakini diplomasia ya Sudan ilipinga majaribio haya yote, ambayo amejiepusha kuyafichua kwa sababu ya vita vya ndani vinavyoendelea nchini humo.

Kuhusu hatua za kurejeshwa uanachama wa Sudan katika Umoja wa Afrika tangu Oktoba 2021, Salem amesema kuwa nchi yake inahisi kukatishwa tamaa na msimamo wa Umoja huo, ambao uliharakisha kusimamisha uanachama wa Sudan kabla ya kutuma ujumbe wa kutafuta ukweli. Amesema Khartoum imeongeza juhudi zake na nchi marafiki kurejesha uanachama, na kwamba maendeleo yamepatikana katika mwelekeo huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan pia amezungumzia mipango ya amani ya kukomesha vita nchini mwake na kusema Khartoum iko wazi kwa juhudi zozote za dhati katika uwanja huo, na kwamba Serikali imewasilisha mpango wa kukomesha vita katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Salem amesisitiza kuwa serikali ya nchi yake “haitakubali nchi inayowaunga mkono waasi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na kuwapa silaha na mamluki wa kigeni kama mpatanishi,” na imewajulisha wapatanishi kwamba mpango wowote ambao haukidhi matakwa ya watu wa Sudan hautasonga mbele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *