LICHA ya mwenendo usioridhisha wa African Sports ‘Wanakimanumanu’ msimu huu katika Ligi ya Championship, kocha mkuu wa timu hiyo, Ally Salimu Mdoe ‘Bai’ amesema moja ya rekodi asiyoitaka itokee ni kuona kikosi hicho kinashuka daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bai amesema licha ya kuichukua timu hiyo katika mazingira magumu ya nafasi iliyopo kwa sasa, ataendelea kupambana na kuonyesha uwezo wake kwa kushirikiana na wachezaji waliopo, ili kuepuka kuishusha daraja.

“Mazingira niliyoikuta timu kila mmoja anayajua, hayakuwa ya kufurahia kutokana na mwenendo wake kwa jumla, hata wakati nilipopewa jukumu hili nililichukua kwa sababu napenda sana kukabiliana na changamoto za namna hii,” amesema Bai.

Bai aliyeifundisha African Sports ikiwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016, kabla ya kushuka daraja, amekuwa kocha wa tatu msimu huu kukifundisha kikosi hicho baada ya Sharifu Joseph Ndokezi na Khalid Adam.

Kocha huyo anayemiliki akademi ya Makorora ya Tanga, huku akiifundisha pia Tanesco sasa B19 FC, anapambana kuinusuru timu hiyo isishuke daraja na iko nafasi ya 14 na pointi 14 kabla ya mechi ya jana dhidi ya KenGold.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *