Mwanza. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Seif Shekalaghe kuchunguza na kukagua kitengo cha wagonjwa wa ndani upande wa wodi za wanaume katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa madai ya wagonjwa kukaa muda mrefu bila kuona madaktari bingwa hadi wengine kufariki dunia.

Mchengerwa ameagiza leo Jumapili, Mei 3, 2026 alipokuwa akifungua kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Mwanza.

Akizungumzia umuhimu wa lugha rafiki na huduma bora kwa wagonjwa zinavyoweza kuwaponya, Mchengerwa amesema kuna malalamiko Muhimbili baadhi ya wagonjwa wanakaa muda mrefu bila kuona madaktari bingwa au bobezi.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza na watumishi wa Afya jijini Mwanza katika kikao chao Cha Baraza kuu la wafanyakazi. Picha na Saada Amir

“Kwa mfano pale Muhimbili kuna kitengo cha wagonjwa wa ndani upande wa wodi za watu wazima…kuna wagonjwa pale toka wameingia hawajamuona daktari bingwa au daktari bingwa bobezi…wengine wanakaa miezi na miezi, wengine mpaka wanafariki…

“Lakini yupo mgonjwa aliyefariki kwa sababu hatukuwahi kumpatia dawa ya sukari…sukari ilikuwa 27 kama tungemuwahi tukatumia lugha nzuri na kumuwahi angepona,” amesema Mchengerwa.

Amesema kuna vifo vingine inawezekana kuvizuia kwa kurekebisha lugha za watumishi wa afya, kuwakimbilia wagonjwa na kuwahudumia.

“Kitengo hiki mwende mkakague, na mimi nitakwenda usiku wa manane nitafanya ziara pale Muhimbili wala sitawaambia lini lakini nitakwenda,” ameeleza.

Amesema ziara zake nyingi ni zakutangaza lakini hatotangaza kwenda hospitalini hapo bali atakuwa anakwenda kimyakimya.

“Watanzania wanamatumaini sana na Serikali hii lakini pia Watanzania wana imani kubwa sana na sekta ya afya, kwa hiyo wajibu wetu ni kufanya kazi kwa bidii,” amesema.

Baadhi ya  watumishi wa Afya wakimsikiliza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza jijini Mwanza katika kikao cha Baraza kuu la wafanyakazi katika wizara hiyo. Picha na Saada Amir

Amesema mpango wa ongea na Waziri umesaidia sana huku akisoma baadhi ya ujumbe zilizotumwa na wananchi ukiwamo wa malalamiko ya huduma katika hospitali hiyo.

“Huyu anasema wagonjwa waliopo wodini Mwaisela ambao wanatumia oksijeni wanashindwa kupelekwa vipimo vya radiolojia mfano X Ray na CT scan kutokana na uhaba wa mitungi ya gesi,” amesoma ujumbe na kuuliza “Najiuliza tumeishiwa kweli mitungi ya kkseji?

Mtuma ujumbe huyo amesema hali hiyo inasababisha ucheleweshwaji wa vipimo vya radiolojia hasa wenye tatizo la upumuaji huku Waziri Mchengerwa akisisitiza changamoto hiyo ipo hawezi kuambiwa haipo akakubali.

“Mwingine akasema uwajibikaji wa watumishi..hapohapo bado nipo Muhimbili ila wagonjwa wanazungushwa kupata huduma lakini mwingine akashauri safari za makambi hospitali zinabaki bila maspecialist wa kutosha kwahiyo hili Katibu Mkuu mkaliangalie,” amesoma ujembe na kuelekeza.

Amewaonywa watumishi sekta ya afya kuwa hatofumbia macho malalamiko ya wananchi wanaolalamikia sehemu mbalimbali ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *