
Unguja. Watu watatu wamenusurika kufariki dunia baada ya jengo lililopo Mji Mkongwe, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi kuporomoka wakiwa ndani.
Tukio hilo limethibitishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Moh’d Ali Abdalla, alipozungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Mei 3, 2026.
Amesema taarifa za kuporomoka kwa jengo hilo ni za kweli na kwamba, kulikuwa na watu watatu ndani wakati tukio hilo linatokea.
“Lakini hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa na hakuna madhara mengine yaliyoripotiwa,” amesema Abdalla.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema tayari amefika eneo la tukio na kuzungumza na wananchi na amewapa elimu juu ya umuhimu wa kuhama kutokana na hatari inayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema katika eneo la Mji Mkongwe kuna majengo 105 ambayo hayako katika hali nzuri; kati ya hayo, amesema majengo 26 yako katika hali mbaya zaidi wakazi wake wanapaswa kuhama mara moja kwa kuwa si salama kwao.
Amesisitiza kuwa wiki mbili zilizopita, ofisi yake ilitoa tahadhari kwa wakazi wa majengo hayo kuondoka na kwenda kwa ndugu, jamaa au marafiki kwa ajili ya usalama wao.
Aidha, amesema baadhi ya wakazi wa jengo lililoporomoka walikuwa tayari wamehama siku moja kabla ya tukio, huku watu watatu waliobaki wakinusurika baada ya kuokolewa wakiwa salama.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wakazi wote wanaoishi katika majengo hatarishi kuhama mara moja ili kuepuka ajali na madhara yanayoweza kuzuilika.