s

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa nchi yake itaanza operesheni maalum ya kusaidia meli zilizokwama katika Mlango bahari wa Hormuz, akieleza hatua hiyo ni kama “msaada wa kibinadamu” kwa mataifa yasiyohusika moja kwa moja na vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

Trump amesema operesheni hiyo itaanza rasmi leo Jumatatu, ikilenga kusaidia meli na wafanyakazi wake ambao wamekwama kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na vizuizi vya Iran katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

Katika ujumbe wake, Trump alisema Marekani itaziongoza meli hizo kupita salama ili ziweze kuendelea na shughuli zao, huku akionya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litakabiliwa na nguvu.

Hatua hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka, ambapo Iran imezuia usafirishaji mafuta na bidhaa zingine kutoka Ghuba ya Uajemi, huku Marekani nayo ikiweka vikwazo kwa meli zinazotoka bandari za Iran.

Wakati huo huo, Iran imethibitisha kuwa imepokea majibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye masuala 14, likijumuisha madai ya kuondolewa kwa vikwazo na kusitishwa kwa mapigano, huku Tehran ikisema bado inalichambua jibu hilo.

Hata hivyo, Trump ameashiria kutoridhishwa na pendekezo hilo la Iran, akisema huenda lisikubalike, wakati Iran ikisisitiza kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo ya nyuklia hadi vita vitakapomalizika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *