Dodoma. Wafanyabiashara zaidi ya 200 waliokuwa wakiendesha shughuli zao kwenye soko la Rehema Nchimbi, jijini Dodoma, wamekataa kuhamia katika soko jipya la Umonga, wakidai malipo ya fidia kutoka kwa Halmashauri ya Jiji hilo.

Madai hayo yanakuja kutokana na kufungwa kwa soko hilo na Halmashauri ya Jiji tangu Oktoba 29, 2025, kutokana na soko hilo kutokidhi baadhi ya vigezo na kuchukuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awali, Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa soko hilo, Abdullah Gogo, ameeleza kuwa eneo la Umonga ambalo wamehamishiwa halijakidhi vigezo, ikiwemo kutokuwa na huduma ya maji na umeme.

Amesema hata eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao lenye ukubwa wa mita za mraba 8,000 limepunguzwa, huku sehemu nyingine ikidaiwa kuuzwa bila maelezo ya kina.

Akijibu malalamiko hayo leo, Jumatatu, Mei 4, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, amesema wafanyabiashara hao wamekuwa wazito kuhamia kwenye eneo jipya la Umonga lililotengwa na Serikali, huku wakieleza kuwa mpaka walipwe fidia.

Gondwe amesema kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, fidia hizo zinatokana na usumbufu walioupata, kudorora kwa uchumi na ugumu wa maisha kutokana na kukosa kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku baada ya soko hilo kufungwa.

“Baada ya soko kufungwa, tuliwapeleka wafanyabiashara kwenye maeneo mengine yenye nafasi, ikiwemo Soko la Job Ndugai, Tambuka Reli na Majengo, lakini walikataa na kuleta mapendekezo ya kulipwa fidia za kusimama kwa biashara zao katika kipindi chote,” amesema Gondwe.

Mbali na madai ya fidia, wafanyabiashara hao pia wameitaka halmashauri hiyo kusitisha matumizi ya utoaji wa mikataba kama kigezo cha kuwapatia nafasi ya kupewa eneo kwenye soko jipya.

Gondwe amesema licha ya sintofahamu hiyo, tayari halmashauri hiyo imeanza kuboresha mazingira katika soko hilo, ikiwemo ujenzi wa vyoo na kugawa maeneo kwa baadhi ya wafanyabiashara ili wajenge vibanda vya muda vya kufanyia biashara zao.

Amesema ugawaji huo utawapatia fursa wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao kwenye eneo moja, huku Serikali ikiendelea kujenga miundombinu wezeshi kwenye eneo lingine kisha kuwapatia wafanyabiashara baadaye.

Gondwe pia amewatahadharisha wafanyabiashara kuacha tabia ya kutoa hongo kwa baadhi ya viongozi wanaowataka kufanya hivyo kwa kigezo cha kuwapatia maeneo bila kufuata utaratibu halali.

“Niwaombe wafanyabiashara kuacha kutoa pesa kwa baadhi ya viongozi wanaowaomba ili wawape maeneo, badala yake wafuate utaratibu sahihi na wa wazi uliowekwa na Serikali,” amesema Gondwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *