Dar es Salaam. Serikali imesifu ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mchango wake katika kuwawezesha wasomi na kukuza ujasiriamali unaoendeshwa na ubunifu nchini kote.
Akizungumza katika uzinduzi Mradi wa Imbeju-UDSM Startup Challenge 2026, ambao umefanyika leo Mei 5, 2026 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ushirikiano huo ni mfano bora unaolenga kuziba pengo kati ya maarifa ya kitaaluma na uhalisia wa utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika maisha ya kila siku.
“Ushirikiano huu unaakisi mwelekeo tunaoutaka kama Taifa ambapo vyuo vikuu vinakuza maarifa na ubunifu pamoja na ujasiriamali na ujuzi wa vitendo unaozalisha thamani ya kiuchumi,” amesema Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda amewahimiza vijana kuwa wabunifu jasiri na wenye nidhamu katika utekelezaji wa mipango yao akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na UDSM utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga kizazi cha wabunifu kitakachochochea mageuzi ya kiuchumi nchini.
“Mpango wa Imbeju ni njia ya kuelekea kwenye Taifa linalojitegemea, ambapo wasomi wetu wanakuwa wabunifu wa ajira, viwanda na suluhisho,” amehitimisha Profesa Mkenda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (wa pili kulia) akipata maelezo ya trekta lililotengenezwa na mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye maonyesho yaliyofanyika wakati wa uzinduzi wa IMBEJU-UDSM Startup Challenge 2026, mradi unaotekelezwa kwa pamoja kati ya CRDB Bank Foundation na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa (wa pili kushoto), Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa wa COSTECH, Dk Amos Nungu.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa dirisha hilo la uwezeshaji wa miradi ya wasomi, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesisitiza dhamira ya taasisi hiyo kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuleta mageuzi jumuishi ya kiuchumi.
“Kwa kutoa mtaji wezeshi unaomudu gharama na kuwezesha ubunifu, tunafadhili biashara na kujenga msingi imara wa uchumi kwa kizazi cha sasa na Tanzania ya kesho,” amesema Tully.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, CRDB Bank Foundation imewafikia zaidi ya wanawake na vijana wajasiriamali milioni 1.75, na kutoa zaidi ya Sh21 bilioni kusaidia ukuzaji wa biashara katika sekta mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Dk Amos Nungu amesema kuna umuhimu wa kubadili tafiti kuwa biashara.
“Mpango huu ni njia ya kujenga kampuni changa zinazoweza kufadhiliwa zinazotokana na sayansi, teknolojia na ubunifu. Unalenga moja kwa moja kuziba pengo la muda mrefu kati ya tafiti na uendelezaji wa kibiashara,” amesema Dk Nungu.
Maombi ya kushiriki katika shindano hili sasa yamefunguliwa, huku dirisha la siku 30 litakalodumu hadi Juni 2026 likiwa wazi kwa wanafunzi na wahitimu wa ndani ya miaka mitano iliyopita wakitakiwa kuwasilisha mawazo yao ili kuwa kwenye nafasi ya kunufaika na mtaji wezeshi kutoka CRDB Bank Foundation.
Washiriki watakaochaguliwa watapata mafunzo, uangalizi wa kitaalamu (mentorship), fursa za ufadhili na masoko.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema ana furaha kuona safari iliyoanza kama ndoto sasa inatimia.
“Kwa ushirikiano huu, tutaanza kuona wajasiriamali wakubwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwahudumia Watanzania kwa ubunifu wao. Kwa muda mrefu hatukuwa na mdau wa kutusaidia kuyageuza mawazo na matokeo ya utafiti wetu kuwa bidhaa inayoingia sokoni, lakini sasa tumempata mbia wa uhakika, CRDB Bank Foundation,” amesema Profesa Anangisye.