Musoma. Watumiaji wa barabara ya Musoma–Busekelea katika eneo la Nyasahungu wilayani Musoma mkoani Mara wanalazimika kutumia kati ya Sh1,000 hadi 3,000 kwa ajili ya kuvushwa baada ya daraja katika eneo hilo kufurika maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Kufurika kwa daraja hilo kumesababisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kuahirisha ziara ya kwenda kukagua shughuli za uchimbaji wa dhahabu na kuzungumza na watumishi pamoja na wachimbaji wadogo katika vijiji vya Seka na Mabui Merafuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

Wakizungumza katika eneo hilo leo Jumatatu, Mei 5, 2026, baadhi ya wakazi pamoja na watumiaji wa barabara hiyo wamesema daraja hilo limekuwa likifurika mara kwa mara hasa nyakati za mvua, hivyo kuwaathiri kiuchumi na kijamii.

Joyce Sadani amesema kutokana na daraja hilo kufurika, magari ya abiria yanapofika katika eneo hilo abiria wanalazimika kushuka ili waweze kuvushwa, jambo ambalo limekuwa kero kwao.

“Mbali na nauli ya gari, ukifika hapa unavushwa kwa kati ya Sh1,000 na Sh2,000 kwa kushikwa mkono na kutembea ndani ya maji, na kwa yule anayechagua kubebwa mgongoni analipia Sh3,000,” amesema.

Amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha watumiaji hao kuingia gharama mara mbili, huku akiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili kuondokana na adha hiyo.

Naye Juma Malima amesema eneo hilo limekuwa kero kwa zaidi ya miaka 15 na kwamba ni muda muafaka sasa suluhisho la kudumu lipatikane ili wananchi na watumiaji wa barabara hiyo waweze kuondokana na adha hiyo.

Baadhi ya watumiaji wa barabara ya Musoma- Busekekela wakivuka katika daraja la Nyasahungu baada ya daraja hilo kufurika kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.  Picha na Beldina Nyakeke

“Wanafunzi wanapata wakati mgumu sana kuvuka hapa kwenda shuleni, lakini pia tukitaka kuvuka kwenda sokoni upande wa pili ni changamoto. Hizi gharama za ziada tunashindwa kuzimudu ukizingatia na hali zetu za kiuchumi siyo nzuri. Serikali isikie kilio chetu,” amesema.

Amesema hali inakuwa mbaya zaidi pale ambapo kunakuwepo na mvua nyingi, ambapo wanafunzi wanalazimika kuacha kwenda shuleni kutokana na kuhofia usalama wao, hali ambayo imekuwa ikiwaathiri kitaaluma.

Aidha, Songoro Ekingo amesema hali hiyo pia imekuwa kikwazo kwao kiuchumi kwani daraja linapofurika wafanyabiashara wanashindwa kusafiri kwenda kununua au kuuza bidhaa zao katika masoko yaliyopo jirani.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema Serikali inatambua changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara ndani ya mkoa huo na tayari hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa ili kutatua changamoto hiyo.

“Ziara ya leo mbali na kwenda kwa wachimbaji wa madini, lakini pia tulikuwa tunazunguka kukagua hali ya miundombinu ya barabara, na hii ni moja ya barabara yenye changamoto na iko kwenye mpango wa matengenezo wa muda mfupi na muda mrefu,” amesema.

Amesema tayari utaratibu wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara umeanza, utaratibu ambao hapo awali ulisitishwa baada ya mkandarasi aliyepatikana kuonekana kutokidhi vigezo, hivyo Serikali kuamua kumtafuta mkandarasi mwingine.

“Hapa kuna mpango wa muda mrefu ambao unahusisha ujenzi wa madaraja mawili, moja katika eneo hili la Nyasahungu na lingine kule katika eneo la Suguti, na taratibu zimeanza. Tunataka kero kama hizi zipate ufumbuzi wa kudumu ili wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo,” amesema.

Kanali Mtambi amewataka wakazi wa mkoa huo kuchukua tahadhari nyakati hizi za mvua ili kuepuka madhara, ikiwemo vifo vinavyoweza kutokea kutokana na kufurika kwa mito na madaraja mkoani humo.

“Kama hakuna sababu ya msingi kusafiri ni vema ukaahirisha safari, na kama ni lazima basi ukikuta pamefurika ni vema usubiri kwanza maji yapungue ndipo uendelee na safari. Hakuna haja ya kuwa na haraka halafu ukapata shida,” amesema.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Musa Kaswahili amesema tayari Serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ya Musoma–Busekelea yenye urefu wa kilomita 88, ambapo ujenzi wake utafanyika kwa awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza itakuwa ni ujenzi wa kilomita 44 kwa kiwango cha lami, ambapo zabuni hiyo inatarajiwa kufungwa Juni 4, 2026 kwa ajili ya hatua nyingine baada ya kutangazwa kwa mara ya pili Mei 4, 2026, tayari kwa hatua nyingine.

“Kwa sasa kulingana na hali ilivyo, tumeamua kujenga madaraja ya muda katika eneo hili la Nyasahungu na pale Suguti wakati mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ukiendelea, na tumepanga kuwa haya madaraja tunayotarajia kuanza kujenga muda si mrefu ndiyo yatakayokuwa kwenye mradi mkubwa ukianza,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *