KOCHA wa Mashujaa, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema ushindi walioupata dhidi ya TRA United ni kichocheo kitakachowarudishia ari ya kujiamini wachezaji, akiamini wanaanza kurejea kwenye kiwango baada ya kupitia kipindi kigumu cha sare.
Julio ambaye alianza kazi ya kukiongoza kikosi hicho Februari 13, 2026, huku akipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, mpaka sasa hana rekodi ya kupoteza zaidi ya kuambulia sare tano mfululizo kabla ya juzi kushinda mara ya pili kwa bao 1-0 dhidi ya TRA United.
Kocha huyo alieleza kuwa matokeo hayo yamefungua ukurasa mpya kwa kikosi chake, kwani morali ya timu imepanda na sasa lengo ni kuhakikisha wanajenga mwendelezo wa matokeo chanya.
“Ushindi huu ni muhimu sana kwetu, umetupa hali ya kujiamini na sasa wachezaji wameanza kutamani kuendelea kushinda baada ya zile sare nyingi tulizopata,” amesema Julio.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Namungo, Julio amesema ataweka mkazo mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji ili iweze kutumia vyema nafasi wanazozipata.
“Tukienda kucheza na Namungo, tunataka kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji ili tuweze kutumia nafasi nyingi tunazopata,” amesema.
Kwa upande wa safu ya ulinzi, kocha huyo alikiri kuona dalili nzuri za maendeleo, akisema wachezaji wameanza kucheza kwa nidhamu na kuelewana vizuri uwanjani.
“Eneo la ulinzi linaonyesha maendeleo mazuri, wachezaji wanacheza kwa nidhamu lakini bado natamani kuona utulivu huo unaendelea,” amesema.
Julio alionyesha kufurahishwa na kiwango cha washambuliaji hasa baada ya Ismail Mgunda kufunga bao zuri mchezo uliopita.
“Nimefurahishwa kuona washambuliaji wangu wanaanza kufunga, Ismail Mgunda alifunga bao zuri sana jana, hii ni ishara nzuri kwetu kwamba kuna matunda ya mabadiliko yanaanza kuonekana mapema,” amesema.
Mashujaa itakuwa ugenini dhidi ya Namungo Ijumaa ya Mei 8, mwaka huu, saa 12:30 jioni katika mwendelezo wa ligi hiyo.