
Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya ipo mbioni kukamilisha mradi wa Soko la kisasa la Matola na Kituo cha Mabasi cha Kimataifa kwa ajili ya mabasi ya mkoani ikiwa ni juhudi za kukamilisha miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa wananchi.
Imeelezwa ujenzi wa miradi hiyo unakwenda kufungua fursa za kiuchumi katika Mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani, hususan mazingira rafiki ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justine Kijazi, ameliambia Mwananchi Digital Mei 4, 2026, alipokuwa akieleza hatua za utekelezaji wa miradi hiyo, hususan maboresho ya miundombinu ya masoko.
Amesema zaidi ya Sh27 bilioni zimetumika kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa soko la kisasa la Matola na kituo kikuu cha kimataifa cha mabasi ya mikoani katika eneo la Old Airport, Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Ujenzi wa soko la kisasa la Matola na kituo kikuu cha kimataifa cha mabasi ya mikoani umefikia asilimia 75, lakini tunatarajia ifikapo Juni 2026 utakamilika na wananchi kuanza kunufaika,” amesema.
Kuhusu manufaa
Kijazi amesema mradi ukikamilika utachangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu yenye mazingira mazuri ya kuvutia na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi na mataifa mbalimbali.
“Upande wa kituo cha kisasa cha mabasi ya mikoani, tunategemea kuongea na majiji ya nchi jirani kujenga ushirikiano wa kibiashara kwa kufungua milango ya fursa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuja kununua bidhaa ndani ya nchi,” amesema.
Kuhusu idadi ya magari
Amesema wastani wa mabasi ya masafa marefu na mafupi 175 yataingia kwa wakati mmoja, huku daladala 80 zikishuka na kupakia abiria ndani ya kituo hicho.
“Tunashukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaokwenda kufungua fursa za kiuchumi sambamba na uwepo wa huduma mbalimbali muhimu, hususan za kifedha, afya na migahawa ya kimataifa,” amesema.
Kuhusu soko la kisasa la Matola, Kijazi amesema likikamilika litaongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka 452 hadi 1,000 kwa wakati mmoja.
“Tunaona Serikali imefanya uwezeshaji mkubwa ambao umeleta mabadiliko makubwa na taswira ya kuvutia kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi,” amesema.
Miundombinu ya barabara, mitaro na masoko
Amesema halmashauri imeweka mikakati kwa robo ya tatu kuboresha miundombinu ya barabara, mitaro na masoko, likiwemo soko la Nsalaga Uyole.
“Tutaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali kupitia fedha za mapato ya ndani. Lengo ni kuwezesha jamii kutoka eneo moja kwenda lingine na kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na mapato ya Serikali,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kijazi amesema kufuatia uwekezaji wa Serikali kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo, ni wakati sasa kwa vijana kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10 ili kuwa na miradi ya kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa, amesema wataendelea kuboresha huduma muhimu na kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Kauli za wajasiriamali
Tausi Azory, mjasiriamali katika Soko la SIDO, amesema wana sababu za kuishukuru Serikali kwa maboresho ya miradi ya soko na kituo cha mabasi kwani maeneo hayo ni muhimu kwa mikusanyiko ya vijana wanaotafuta ajira.
“Kimsingi hatua hiyo ya Serikali ni kubwa, ambayo itatuwezesha kuongeza fursa za kiuchumi kwa kuuza bidhaa usiku na mchana kupitia uwekezaji huo,” amesema.