Dodoma. Mbunge wa Kinondoni Tarimba Abbas amesema Jiji la Dar es Salaam bado lina shida ya maji licha ya kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa).

Amesema Dawasa kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Mkama Bwire wamekuwa wakipambana kuhakikisha wananchi wanapata mjisafi na salama.

Abbas ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 5,2026 wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo ametaja maeneo yenye changamoto kubwa ya maji.

Tarimba amezitaja kata za Mzimumi, Tandale, Ndugumbi, Nanasifu, Makumbusho, Mwananyamala, Kigogo, Magomeni, Kinondoni na Kijitonyama.

Hata hivyo, Tarimba amesema kuwa Dawasa inahitaji kusaidia ili iweze kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa mahitaji ya maji ni makubwa.

“Maji yanayotakiwa Dar es Salaam ni zaidi ya lita 772 milioni kwa siku, lakini yanayozalishwa ni lita 553.7 milioni kwa siku ambapo upungufu ni lita 259 milioni. Dawasa wanafanya kazi kubwa, lakini bila kusaidiwa itakuwa uongo,” amesema Abbas.

Pia, amesema maji yanayozalishwa hayafiki yote katika Jiji hilo lenye idadi kubwa ya wakazi kwa kuwa, bado kuna changamoto ya upotevu wa maji.

Amesema asilimia 49 ya maji yanayozalishwa yanapotea kutokana na kuchoka kwa mitambo ingawa, amesema ipo mitambo mipya imepelekwa lakini ufungaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.

Kutokana na hilo, Tarimba amependekeza utengenezwe utaratibu wa jinsi ya kuondoa upotevu wa maji angalau kwa ufikie asilimia 25.

Kwa mujibu wa Abbas, mitambo inayosukuma maji Dar es Salaam ni ya tangu 1960 na mingine imejaa kutu kutokana na kukaa muda mrefu akaomba zikopwe fedha ili kuibadilisha.

Amesema maji ni dini, siasa, maisha na kila kitu kitu akitumia kauli ya Waziri Aweso kuwa maji hayana mbadala.

Kuhusu Bwawa la Kidunda amesema mradi umeanza 2023, lakini hadi sasa ni asilimia 47 wakati imebaki miezi minane akihofu huenda kazi haitakamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *