
Dodoma. Zaidi ya wanasayansi na madaktari 170 kutoka mataifa nane duniani wanakutana jijini Dodoma kwenye Kongamano la Sayansi ya Upandikizaji Viungo Tanzania ili kujadili na kutoa mapendekezo kuhusu ubora na umuhimu wa huduma hizo.
Kongamano hilo litaongozwa chini ya wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ambapo nchi za Italia, Uganda, Nigeria, Singapore, Japan, India na Afrika Kusini wamethibitisha kushiriki huku Uingereza akithibitisha ushiriki kwa njia ya Mtandao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mei 5,2026, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profes Abel Makubi amesema kongamano hilo ni muhimu na linakuja na matokeo chanya kwa Taifa.
Profesa Makubi ametaja miongoni mwa huduma zitakazojadiliwa ni upandikizaji figo, upandikizaji uroto na maandalizi ya kuanza kupandikiza moyo na ini mambo aliyosema yanahitaji wataalamu kujadili na kubadirishana uzoefu.
“Kongamano hili ni la kisayansi ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamini Mkapa, lakini mtambue kuwa kongamano hili litawaleta pamoja Wizara ya Afya, baadhi ya Taasisi na Hospitali za Kanda,”amesema Profesa Makubi.
Amesema watajadili mikakati ya mbele ya utoaji huduma za upandikizaji viungo nchini Tanzania na kubadilishana utaalamu na ujuzi ikiwemo uzoefu katika Mataifa ambayo yametoa huduma hizo kwa mafanikio katika kipindi kirefu.
Mkurugenzi amesema huduma za upandikizaji zina gharama kubwa hivyo kukutana kwao kunakwenda kujadili wanaweza kufanya kazi kwa gharama za chini ili waweze kuwahudumia wahitaji.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi, gharama za kupandikiza figo ni Sh40 milioni ambapo hadi sasa Benjamin Mkapa imepandikiza wagonjwa 56 huku watu 50 wakiwa kwenye foleni ya kusubiri huduma hiyo.
Mtaalamu bingwa wa upandikizaji Uroto kwa watoto Dk Stella Malangahe amesema amesema Hopsitali hiyo imeshapandikiza watoto 30 na walioko kwenye orodha wanafikia 30 ambapo gharama kwa mtoto mmoja ni Sh75 milioni.
“Hata hivyo tunapata changamoto ya ufinyu wa miundombinu kwani hivi sasa tunahudumia watoto watatu kwa wakati mmoja lakini mwelekeo wetu angalau tufikie watoto sita kwa wakati mmoja ikiwa tutaongeza vyumba vitatu,”amesema Dk Stella.
Daktari bingwa wa upasuaji Mugisha Nkoronko amesema uwezo wa wataalamu wa ndani kwa sasa unaaminika na ndiyo maana wengine kutoka nje wameanza kuja Tanzania kujifunza.
Dk Mugisha ambaye pia ni rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania, ndiye Mwenyekiti wa kongamano hilo akisema bado kuna nchi zinaendelea kuthibitisha ushiriki wao japo kwa njia ya mtandao kwani wengi wameonyesha imani kwa huduma zinazotolewa nchini Tanzania.